FAMILIA moja katika Kijiji cha Chela, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imesimulia jinsi inavyoishi na fisi kwa miaka 44 sasa.Kijiji cha Chela ndiko alikozaliwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige na fisi hao walionekana hadharani wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipofika katika kijiji hicho akiwa katika ziara mkoani Shinyanga wiki iliyopita. Familia inayofuga fisi hao ni ile inayounda kikundi cha burudani ya ngoma za jadi ambacho ni maarufu katika Kanda ya Ziwa kikijulikana kwa jina la Bununguli na kwamba fisi hao ni moja ya nyenzo za kufanikisha kazi yao. Mmoja wa wanafamilia wanaomiliki ngoma hiyo, Lukondya Mabiti Jinoja anasema aina ya fisi wanaofuga wanajulikana kama nhawa kwa lugha ya Kisukuma na kwamba fisi wa aina hiyo wana maumbo makubwa kuliko wale waitwao mbitimululu wenye maumbile madogo yasiyovutia. Alisema ingawa fisi hao wameanza kuwatumia na kuonekana hadharani siku za karibuni, familia yake imeanza kuishi na wanyama hao tangu mwaka 1968. “Ni miaka mingi inafikia 44 au 45 na katika muda wote huo tumejifunza mbinu mbalimbali za namna ya kuwakamata na tumefanikiwa kuishi nao kwa muda wote bila kupata madhara yoyote,” anasimulia Jinola. Jinoja ambaye ni Mwenyekiti wa Bununguli, alisema wakati wa maonyesho ya burudani za ngoma, fisi hao hutumika kunogesha na kuvutia umati wa watazamaji wa ngoma hizo. Wanawakamataje? Jinola anasema mara nyingi ukamataji wa fisi hao hufanywa kwa kutumia mbinu za kijadi ambazo hata hivyo, hakutaka kuziweka wazi. “Hawa mafisi hukaa kwenye mapango, kwa hiyo sisi huenda tukiwa kundi kubwa kuwavizia taratibu na tukiwakaribia huwa tunawavamia, tukiwakamata tu huwa tunawahifadhi kwenye masanduku yetu makubwa na kuwafungia, kisha huyabeba hadi nyumbani tunakowafuga,” alisema Jinola. Alisema fisi hufugwa kama ilivyo wanyama wengine ambao ni mbwa au paka na kwamba baada ya kuishi nao kwa siku kadhaa, huzoeana nao na baadaye huwa wapole wasiokuwa na madhara kwa binadamu.Hata hivyo, Jinoja alisema changamoto kubwa waliyonayo ni uwezo wa kuwalisha kwani fisi mmoja ana uwezo wa kula kati ya kilo mbili hadi nne za nyama kwa siku moja kulingana na ukubwa wake. “Natumia wastani wa kilo 16 za nyama kila wiki kuwalisha fisi wangu wanne, ni kazi kubwa kweli lakini tunajitahidi kadri tunavyoweza,” alisema.Hata hivyo, alisema baada ya familia hiyo kufanikisha mpango wa kuishi na fisi hao sasa wameweka mikakati wa kufuga chui siku zijazo. Ili kufahamu kwa undani jinsi wanavyowakamata fisi hao na kutumiwa kwenye shughuli za ngoma. |
Saturday, March 3, 2012
Waishi na fisi kwa miaka 44 sasa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment