Saturday, March 3, 2012

SERIKALI YAAGIZA MISHAHARA YA TAZARA ILIPWE HARAKA


Waziri wa Uchukuzi Omari Nundu akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na utendaji kazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) leo katika ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo uliopo jijini Dar es Salaam. Siku za hivi karibuni utendaji kazi wa TAZARA umekuwa wa kusuasua kutokana na matatizo mbalimbali yanayolikabili Shirika hilo. (Picha na Anna Nkinda wa Maelezo)
Baadhi ya watendaji wakuu wa wizara ya Uchukuzi wakimsikiliza Waziri Omari Nundu (hayupo pichani) wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na utendaji kazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) leo jijini Dar es Salaam. Siku za hivi karibuni utendaji kazi wa TAZARA umekuwa wa kusuasua kutokana na matatizo mbalimbali yanayolikabili Shirika hilo. Kulia ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mhandisi Omari Chambo.
Baadhi ya viongozi wa Umoja wa Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU) tawi la TAZARA wakijadili mambo mbalimbali mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa utendaji kazi wa Mamlaka ya TAZARA baina ya Waziri wa Uchukuzi Omari Nundu na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Siku za hivi karibuni utendaji kazi wa Mamlaka hiyo umekuwa wa kusuasua kutokana na matatizo mbalimbali yanayolikabili Shirika hilo.Kutoka kulia ni Lufingo Mwanghba, Bundala Kabulwa, Yassin Mleke na Benjamini Kehogo.

SERIKALI imeigiza menejimenti ya TAZARA kuhakikisha kwamba mishahara ya wafanyakazi wake inalipwa haraka.
Aidha imeongeza kuwa menejimeti hiyo ihakikishe yanapotokea matatizo inayashughulikia na kutoa maamuzi kwa muda muafaka.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu wakati akizungumza na waandishi wa habari leo(jana) jijini Dares Salaam kuhusu utendaji kazi wa TAZARA.
“Changamoto zilizopo hivi sasa ni TAZARA kutoweza kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati na kutokuwa na mafuta kwa ajili kuendesha treni za abiria . hadi jana kuna baadhi ya wafanyakazi hawakuwa wamelipwa mishahara ya Januari na Februari, mwaka 2010 na wote mishahara ya Februari hawajalipwa .
“Kutokana na hali hiyo wizara imeiagiza menejimenti ya TAZARA ihakikishe kwamba ifikapo Machi 2, 2012 mishahara ya Januari iwe imelipwa na mafuta yawe yamepatikana kwajili ya kuendesha angalau treni tano kwa siku. Mishahara ya Februari nayo ilipwe haraka,” alisema Waziri Nundu.
Aliongeza kuwa tayari menejimenti hiyo imekamilisha taratibu za kuingiza fedha za mishahara ya Januari katika benki, hivyo itawafikia wafanyakazi wa Mbeya Machi 3,mwaka huu na mishahara ya Februari ilipwe katikati ya Machi, mwaka huu.
Alifafanua kuwa tayari TAZARA imeshapata lita 600,000 za mafuta , hivyo leo treni nane zimeshanza kufanya kazi kati ya hizo za sita ni za mizigo.
Waziri Nundu alisema mikakati iliyopo sasa ni kuiongezea TAZARA uwezo wa uchukuzi kwa kukarabati injini na mabehewa yaliyopo, kuboresha miundombinu ya reli pamoja na njia za mawasiliano na kuendeleza ushirikiano mzuri wa wateja wakubwa katika kukarabati injini na mabehewa kwa makubaliano maalumu.
Alisema Baraza la Mwaziri la TAZARA limepanga kukutana Mei 23,mwaka huu kujadili masuala ya shirika hilo kwa kina zaidi na kupata ufumbuzi ili kuboresha huduma ziwe za kudumu.
Waziri Nundu aliongeza kuwa atakutana na wafanyakazi wa TAZARA Machi 23, mwaka huu na kukagua shughuli za utendaji kazi na njia ya reli kutoka Dares Salaam hadi Tunduma.

No comments:

Post a Comment