SLAA, MKAPA KUONGOZA MAPAMBANO ARUMERU, NASSARI, SUMARI WAPITISHWA
Na Waandishi wetu, Dar na Arusha
VYAMA vya CCM na Chadema vimetangaza rasmi vita ya kuwania Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha huku vikianika majina ya makada watakaoongoza mapambano kwa ajili ya kujihakikishia ushindi.
CCM ambayo imempitisha Siyoi Sumari kuwania nafasi hiyo, imesema kampeni zake zitazinduliwa na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho ambaye pia alikuwa Rais wa awamu tatu, Benjamin Mkapa na Chadema itawatumia viongozi wake wa kitaifa, wakiongozwa na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.
Wakati huohuo, Kamati Kuu (CC) ya Chadema jana ilimpitisha, Joshua Nasari kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe aliwaeleza viongozi wakuu wa chama hicho, wapenzi na wafuasi wa Chadema waliojazana eneo la Hoteli The Ice Age Usa-River, wilayani Arumeru jana kuwa wamejiandaa kikamilifu kunyakua jimbo hilo na kamwe hawatakubali hujuma zozote kutoka kwa mtu au chama chochote.
Mbowe aliyezungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wake, Dk Slaa kumtanga rasmi Nasari, alitamba kuwa mchakato wa kumtafuta mgombea kupitia chama hicho haujaacha nyufa wala mifarakano miongoni mwa wagombea na wafuasi wao kama ilivyotokea kwa vyama vingine vya siasa ambavyo hakuvitaja.
Alisema mara nyingi mipasuko ndani ya vyama vya siasa hutokana na mchakato wa kupata wagombea kutokana na hila za baadhi ya viongozi, wanachama au wapambe wa wagombea, hali aliyosema haijajitokeza ndani ya Chadema kutokana na mfumo mzuri unaozingatia demokrasia kwa wote bila kujali umaarufu au ukwasi wa mtu.
“Wagombea wote waliojitokeza kuchukua fomu kuomba uteuzi tumewaalika katika Kamati Kuu na wote wameridhika na ushindi na uteuzi wa mgombea mwenzao na wote watashiriki kikamilifu kwenye kampeni kuhakikisha ushindi wa chama unapatikana,” alisema Mbowe.
Akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu, Dk Slaa, alisema kikao hicho kilichoshirikisha wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya zinazoongozwa na Chadema, kwa kauli moja kilipitisha jina la Nasari kuitikia sauti ya wananchi na wakazi wa Arumeru waliomchagua kwa kura 805 kati ya 888 zilizopigwa kwenye kura za maoni.
“Wananchi Arumeru tumesikia kauli yenu kupitia kura zenu za maoni, Nasari ni kijana wenu siyo wa Dk Slaa, Mbowe wala Chadema.
Katika kura za maoni, Nasari alimwacha mbali mgombea wenzake Anna Mghiwa aliyemfuatia kwa kupata kura 23 huku wagombea wengine wanne, wakipata kura chini ya 20.
Chama hicho pia kinaendelea kufanya tathimini ya kutumia helikopta katika kampeni zake katika jimbo hilo.
Nasari ashukuru
Akitoa shukrani mbele ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama chake, Nasari aliwaomba wafuasi, wapenzi na wanachama wote wa Chadema kushikamana na kuwa tayari kwa mapambano ya haki, kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
"Wao (CCM), najua watatumia dola na fedha, lakini sisi tusihofu kwani tuna Mungu anayetupigania kwa sababu mapambano yetu ni kudai haki dhidi ya uovu.
Kwa pamoja tukishirikiana kuondoa hofu kwani tutashinda," alisema Nasari.
CCM
Kwa upande CCM Kamati Kuu (CC) ya chama hicho jana ilimteua Mwenyekiti mstaafu ambaye pia ni Rais mstaafu wa awamu ya Tatu , Mkapa, kuongoza kampeni za kumnadi Mgombea Ubunge wa chama hicho, Siyoi Sumari katika jimbo la Arumeru Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alisema kikao cha kamati hiyo kilichoketi jana, kilipitisha jina la Siyoi kuwania nafasi hiyo iliyoachwa na baba yake, Jeremia Sumari aliyefariki usiku wa Januari 18 mwaka huu.
Nape alieleza kwamba, kamati hiyo pia imemteua Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha ya chama hicho, Mwingilu Nchemba kuratibu kampeni hizo.
Katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga ambao CCM ilishinda, Mkapa ndiye aliyefungua kampeni hizo huku, Nchemba akiratibu kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Akizungumzia tuhuma za rushwa ambazo zimekuwa zikiripotiwa katika mchakato wa uteuzi, aliitaka Takukuru kuhakikisha wanakamata mtandao mzima uliohusika na utoaji rushwa.
Kauli ya Siyoi
Sumari, aliambia Mwananchi Jumapili kuwa kwamba pamoja na kufurahishwa na uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kupitisha jina lake kupeperusha bendera ya CCM wilayani Arumeru Mashariki, chama hicho kinapaswa kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha kinatetea jimbo hilo.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba changamoto zote alizozipitia katika mchakato wa uteuzi , zikiwemo tuhuma mbalimbali za rushwa ni misukosuko ya kisiasa ambayo haiwezi kuepukwa zaidi ya kukabiliana nayo.
“Nashukuru chama kwa kupitisha jina langu, lakini changaomoto zote nilizokuwa nikipitia naamini ni misukosuko tu ya kisiasa, lakini tusahau yaliyopita sasa tusonge mbele kunyakua ushindi,” alisema Sumari
UVCCM
Katika hatua nyingine Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM ) wilayani Arumeru, imefurahishwa na uamuzi uliofanywa na CC ya CCM kumpitisha Siyoi kupeperusha bendera ya chama hicho na kueleza kwamba kilio cha wanachama wa CCM wilayani humo, sasa kimesikilizwa.
Hata hivyo, wakati jumuiya hiyo ikiupokea ushindi huo kwa furaha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) imeendelea na kamata kamata yake ambapo safari hii ilimshikilia na kumhoji kwa muda Katibu Hamasa wa umoja huo wilayani Arumeru Mashariki, John Nyiti kisha kumwachia huru.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Esther Maleko alisema mbali na kilio cha wakazi wa jimbo hilo kusikika juu ya mgombea wao, umoja wao umejipanga kikamilifu kuingia ulingoni kuhakikisha ushindi unapatikana.
Hekaheka za uchaguzi wa jimbo hilo wakati zikiendelea baadhi ya makada wa CCM na UVCCM wilayani humo wameendelea kukumbwa na misukosuko baada ya viongozi wake akiwemo Nyiti kushikiliwa na Takukuru kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa wilayani humo.
Nyiti alipoulizwa juu ya taarifa hizo kwa njia ya simu alikiri kukamatwa na maofisa wa Taasisi hiyo.
Kamanda wa Takukuru mkoani Arusha, Mbengwa Kasumambuto alipoulizwa na gazeti hili juu ya taarifa hizo hakuweza kukiri wala kukataa juu ya kuhojiwa kwa kada huyo na kudai kwamba wanaohojiwa na Taasisi hiyo wako wengi na wengine wanahojiwa kama mashahidi, hivyo alidai si vyema kuwataja majina kwa kuwa bado wanakamilisha uchunguzi wao.
Hali ilivyo ndani ya vyama
Makundi ya vigogo wa CCCM ambao wanajipanga kugombea Urais mwaka 2015, yametajwa kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho katika uteuzi wa mgombea wa Ubunge Arumeru Mashariki.
Mpasuko wa makundi hayo, inaelezwa unaweza kuchangia chama hicho kupoteza jimbo hilo.
Sumari amekuwa akiungwa mkono na kundi la Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa huku wagombea wengine, walikuwa wakiungwa mkono na kundi la na vigogo wa chama hicho wanaojipambanua kuwa ni wapiganaji dhidi ya ufisadi...Soma zaidi www.mwananchi.co.tz
Waliojitoa CUF waanzisha ADC |
ALIYEKUWA Meneja wa Kampeni za Urais wa CUF mwaka 2010, Said Miraji na
wenzake jana waliwasilisha rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa maombi ya
usajili wa muda wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).
Juzi,
Miraji na aliyekuwa mgombea ubunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF, Adawi Limbu
walijitoa chama hicho na kutangaza kusudio la kusajili chama kipya.
Jana, ujumbe wa chama hicho uliwasili katika Ofisi ya Msajili, Dar es Salaam saa 7:30 mchana ukiongozwa na Miraji ambaye alijitangaza kuwa ni Kaimu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wake, Limbu na kupokewa na Wangalizi wa Ofisi ya Msajili, Galasia Simbachawene. Akizungumza na viongozi hao, Simbachawene alisema kulingana na taratibu za usajili wa vyama, maombi ya chama kabla ya kuwasilishwa kwa msajili yanahitaji kupatiwa muda ili yapitiwe na maofisa mbalimbali akiwemo Mwanasheria wa Ofisi ya Msajili. “Nimepokea maombi. Msiwe wasiwasi yameshafika kwa Msajili. Utaratibu uliopo ni kwamba maombi yanapokewa na kupewa muda zaidi wa kuyapitia kwa kushirikiana na mwanasheria ili kuona kama yamekamilika baada ya hapo yatawasilishwa rasmi kwa Msajili,” alisema Simbachawene. Vitu vilivyowasilishwa jana ni barua ya maombi ya usajili, rasimu ya katiba ya chama iliyoambatanishwa na hati ya kwenda kwa msajili (PF1) pamoja na hati ya kiapo ya kuwa chama cha jamii chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992. Miraji alisema wameamua kuanzisha chama hicho baada ya kutoona chama chochote cha siasa kinachowafaa kujiunga akisema karibu vyote vinafanana tabia. “Tumeamua kuanzisha chama cha siasa lakini, kitajikita kijamii zaidi. Hatujafanya uamuzi wa kishabiki kwani siasa za nchi hii zilivyo, si rahisi mtu kutoka chama kimoja kwenda kingine kwani vyote vinafanana, vina maneno matamu sana hasa CCM ,” alisema Miraji. Alisema ili kupata maoni ya wananchi kuhusu katiba ya chama hicho, rasimu ya katiba hiyo itaingizwa kwenye mitandao ya kompyuta pamoja na magazeti na majarida na kusambazwa katika maeneo mbalimbali. “Hatupo tayari kuwa na katiba ya mtu mmoja wala watu 100 tu, lazima tukusanye maoni ya muundo wa katiba kutoka kwa watu mbalimbali kupitia mitandao na kutoa matangazo kwenye magazeti yatakayoweza kuwafikia watu katika maeneo yote,” alisema Miraji. Alisema katika katiba ya chama chao vitu walivyozingatia ni pamoja na ukomo wa madaraka na kuweka kamati maalumu ya usuluhishi ambayo haitawahusisha viongozi wa juu wa chama ili kuepeka kuwafukuza wanachama wanapofanya makosa ambayo yanaweza kurekebishika. Kwa upande wake, Limbu alisema wananchi wanapaswa kuwa macho na vyama taasisi kwani viongozi wa vyama vya siasa wanafanya vyama hivyo kama mtaji. “Chama hiki hakina mwenyewe watu wanaruhusiwa kuja kujiunga wasisubiri mpaka wafukuzwe katika vyama vingine ambavyo havijui umuhimu na thamani ya wanachama,” alisema Limbu. Limbu aliwataka wanasiasa walio kwenye vyama visivyo na msimamo kuhamia chama hicho ili waweze kutetea haki za wananchi na kuwapa mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Walikitabiria kifo CUF Walipokuwa wakitangaza kujitoa CUF, Miraji na mwenzake walikitabiria kifo cha chama hicho wakisema kimepoteza mwelekeo kutokana na kuongozwa na watu wanaodhani ni mali yao. Pia walimshutumu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro wakisema ameamua kwa makusudi kukiua.Hata hivyo, Mtatiro alijibu tuhuma hizo akisema, “Said Miraji ni mfuasi wa Hamad Rashid kwa muda mrefu sana. Amekuwa akikihujumu chama yeye na Hamad Rashid, kuondoka kwake siyo tishio la CUF. Nafahamu anakwenda kukabidhiwa chama na Hamad Rashid kama kaimu mwenyekiti hadi Hamad atakamoliza ubunge wake, tunamtakia kila la heri katika kujitoa CUF.” |
Maswali ya kujiuliza ni mengi juu ya siasa za bongo.
Wengi watajiuliza tulipotoka ni wapi, tulipo ni
wapi na ni wapi tunaelekea tukijua fika Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kwa neema
ya rasilimali watu na mali, lakini bado tu maskini wa fikra na tajiri wa
rasilimali.
Blog hii inalengo kubwa na kutoa fursa ya
kubadilishana mawazo wewe na watanzania wengine juu ya mstakabali wa siasa zetu
na ni kwakiasi gani tutasaidiana kutoka hapa tulipo. Pamoja na hayo, kuangalia
kwa undani aina ya siasa, uchumi na mipangilio ya kijamii ambayo, kama
tutaipangilia, itatusaidia kufanya mipango ya kimaendeleo kwa uharaka na kuondoa
umaskini uliokidhiri kwa kiasi cha watu kifikiria ni sehemu ya maisha
yetu.
Tuwe na lengo la kutafuta njia za kusimamia
siasa na taratibu za nguvu na mamlaka ambazo zitasaidia kufanya kazi kwa ufanisi
zaidi yazilizopo. Tunataka kufanya hivyo kwa msingi wa umakinifu kwa yale
yaliyofanyika vizuri kwa sasa na huko nyuma toka enzi ya Baba wa taifa, Hayati
Mwalimu Julius K. Nyerere, kufuatiwa na Mweshimiwa Ali-Hassan Mwinyi, Mweshimiwa
Benjamin Mkapa na Mweshimiwa Raisi, Jakaya Mrisho Kikwete.
Karibu kwenye blog hii! Kazi yetu kubwa ndio
hii inaanza, lakini tunapendelea kubadilishana mawazo, elimu, ujuzi, fikra na
watu wenyewe uelewa mkubwa wa kufikiri na wahamasishaji ambao fikra zao
zinashirikiana katika kuendeleza vizuri siasa za bongo, moja ya changamoto kubwa
Tanzania
No comments:
Post a Comment