Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Dk. Terezya Huvisa ameiasa jamii ya
watanzania kujenga tabia ya kupanda na kutunza miti ili kufaidika na biashara ya
hewa ukaa.
Dk. Huvisa
ameyasema hayo mwishoni mwa wiki katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa
alipofanya ziara ya kikazi kukagua miradi inayotekelezwa na Kampuni ya Green
Resources katika vijiji vya Idete na Uchindile
Amezitaja faida
za misitu kuwa ni uuzaji wa hewa ukaa ambayo kwa kiasi kikubwa hupatia wananchi
fedha kwa ajili ya huduma muhimu za maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
shule, zahanati, na kutoa ajira kwa jamii inayozunguka.
Dk. Huvisa
amewasihi wananchi wa Mufindi kutumia utaalamu wa wawekezaji hao katika kuandaa
mashamba yao ya miti na kudumisha uhusiano mzuri baina yao na wawekezaji.
“msiuze ardhi yenu yote kwa wawekezaji bali tumieni fursa hiyo kuandaa mashamba
yenu kitaalamu ili muweze kunufaika pia” Alisisitiza Dk.
Huvisa.
Akitoa taarifa
kwa Waziri, Meneja wa Mradi wa Green Resource Bw Sangito Sumari, amesema
kiasi cha Shilingi bilioni moja zimetolewa na kampuni hiyo kusaidia miradi ya
maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Awali, Barabara, na miradi ya
Maji katika vijiji vya Idete, Mapanda, Uchindile, Makungu na
Chogo.
Kuhusu biashara
ya hewa ukaa katika mwaka 2010, “Kampuni imetoa asilimia kumi kwa ya mauzo ya
hewa hiyo kwa vijiji vya wilaya ya Mufindi na Kilombero ambapo kijiji cha Chogo
kilipata sh. Milion 10 , Mapanda milioni
30, Uchindile Milioni 75 na Kitete 10 milioni,” alisisitiza Bw.
Sumari.
Kampuni ya Green
Resources inafanya kazi zake katika nchi ya Tanzania, Uganda na Msumbiji na
inajishughulisha na upandaji wa miti, uvunaji wa hewa ukaa na mradi wa kuzalisha
na kusambaza umeme unaandaliwa.
No comments:
Post a Comment