Na Mwandishi Wetu
KATIKA matamasha ya Pasaka mwaka 2010 na 2011,
yaliyopambwa kwa muziki wa Injili kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es
Salaam, kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, nyoyo za mashabiki zilikongwa na
waimbaji kochokocho waliotumbuiza.
Lakini kivutio kikubwa walikuwa ni mwimbaji wa Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya, Solomon Siaka Mukubwa na Rose
Muhando, ambao mara kwa mara kelele za mashabiki zilisikika wakitaka kila mmoja
aendelee kuwapa burudani.
Mbali ya Rose Muhando ambaye wimbo wake wa Nibebe
uliteuliwa kuwa Wimbo Bora wa Mwaka 2009 kupitia televisheni ya Taifa, TBC1 na
Mukubwa, wasanii wengine walioshiriki na kufanya vizuri ni Flora Mbasha na
Upendo Nkone.
Waimbaji wengine ni Bahati Bukuku, Jennifer Mgendi,
Geraldine Oduor, Enock Jonas, na kundi la muziki wa Injili la Upendo la
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Lakini Mukubwa na Rose ndio waliokuwa kivutio zaidi
kutokana na kushangiliwa kwa nguvu. Mukubwa anasema hamasa aliyoipata mwaka juzi
na mwaka jana ndiyo inampa msukumo zaidi wa kuendelea kukonga nyoyo za mashabiki
katika tamasha la mwaka huu.
Tamasha la mwaka huu litafanyika kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, Aprili 8, kisha litarindima kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini
Dodoma Aprili 9, ambayo itakuwa Jumatatu ya Pasaka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo,
Alex Msama anasema kwa vile tamasha la mwaka jana lilikuwa la mafanikio makubwa,
anaamini mwaka huu watavuka malengo ya kukusanya fedha kwa ajili ya watoto
yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wajane wasiojiweza.
Wasifu wa Mukubwa
Mukubwa ni mlemavu wa mkono mmoja wa kushoto anaodai
umekuwa katika hali hiyo kutokana na kudhuriwa kwa uchawi na mama yake wa kambo
alipokuwa na umri mdogo.
Anasema akiwa na miaka 12, alipata matatizo hayo kwa
kutokea uvimbe wa ajabu na hakuna aliyejua tatizo lilikuwa nini, lakini
walibaini kuwa ni mama yake wa kambo ndiye alimroga kutokana na
wivu.
Mukubwa aliyetamba na wimbo wa 'Mfalme wa Amani',
anabainisha kwamba aliugua kwa miaka mitatu na alihaha huku na huko hospitalini
hadi kwa waganga wa kienyeji kusaka tiba, lakini hakufanikiwa.
Kwa mantiki hiyo, alifikia uamuzi wa kukatwa mkono kwa
vile ulikuwa umeharibika.
Mukubwa anasema mama yake huyo wa kambo alikiri kumroga
baada ya kuokoka, hivyo alimsamehe. Hata hivyo, anasema mkono huo aliokatwa
haumzuii kumuimbia Mungu.
Mukubwa anasema alihamia Kenya kutokana na msaada wa
mwimbaji wa nyimbo za Injili, marehemu Angela Chibalonza, aliyekuwa mshauri
wake.
Mukubwa amezaliwa kwenye familia ya watoto tisa,
wanaume saba na wanawake wawili, yeye akiwa wa kwanza, ameoa kwa alifunga ndoa
na Betty Japhet, Machi mwaka 2010.
Mwimbaji huyo wa nyimbo za kumsifu Mungu mwenye ulemavu
wa mkono mmoja, hivi sasa anatamba na albamu yake mpya ya Usikate Tamaa, ambayo
anaamini itamng'arisha katika tamasha hilo.
Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ya Usikate Tamaa ni
Usikate Tamaa, Mungu Wangu Nitetee, Niko na Yesu, Mke Si Nguo, Moyo Tukuza
Bwana, Chunga Ahadi Yako na Yesu Jina Zuri.
Mukubwa anayeishi Kenya, amewahi kutoa albamu mbili
ambazo ni Sijaona Rafiki na Mungu Mwenye Nguvu.
Sijaona Rafiki Kama Yesu ambayo ni albamu yake ya
kwanza ina nyimbo za Uwe Nami Bwana, Sijaona Rafiki Kama Yesu, Nitayainua Macho,
Matendo ya Mungu, Bwana Wastahili na Yesu Kimbilio.
Albamu yake ya pili ya Mungu Mwenye Nguvu ina nyimbo za
Mungu Mwenye Nguvu, Mkono wa Bwana, Mfalme wa Amani, Siku Moja, Tabia Ina Dawa
na Roho Yangu Ikuimbie.
Wengine watakaoshiriki
Mbali na Mukubwa, wengine waliothibitisha kushiriki
tamasha hilo litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka ni Rose Muhando, Anastazia
Mukabwa, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, Atosha Kissava,
Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka DRC na kundi la Glorious
Celebration.
Pia kwaya mahiri ya Kinondoni Revival inayotamba na
albamu yao mpya ya Mtu wa Nne, inatarajia kutumbuiza katika tamasha la Pasaka.
Mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe.
Nyimbo zilizomo kwenye albamu ya Kinondoni Revival ni
Mtu wa Nne, Imekwisha, Chukua Hatua, Mtafuteni Bwana, New Season, Hakikisha,
Ninakushukuru na Dini Iliyo Safi.
Pia kwaya hiyo ya Kinondoni Revival imewahi kutamba na
albamu yao ya Kilio cha Mcha Mungu yenye nyimbo nane za Kilio cha Mcha Mungu,
Kwanini Unataka Kujiua, Ayubu II, Vumilia Kidogo, Nafsi Yangu, Natamani Kwenda
Mbinguni, Ndugu Yetu Twakutafuta na Twalilia Tanzania ambazo pia wameahidi
wataziimba.
Msama anasema baada ya waimbaji hao kutikisa Uwanja wa
Taifa, mashambulizi mengine yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9
mwaka huu.
Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika
kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida
na viti maalumu sh. 10,000.
Tamasha la Pasaka la mwaka huu pia litashirikisha
waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi za Uganda, Rwanda, Afrika Kusini na
Zambia. Pia kutakuwa na kwaya na vikundi vya burudani.
No comments:
Post a Comment