Monday, March 5, 2012

Shule Zenye Walemavu Zisaidiwe


 Mwalimu Mratibu wa Kituo cha Walemavu cha Shule ya Msingi Iliboru, Loitusho Yamat akionesha hesabu wanazofundishwa baadhi ya walemavu.
Kikundi cha Wanapambazuko Klabu cha Shule ya Msingi Iliboru wilayani Arumeru, kikundi hiki hufanya kazi ya kuelimisha jamii.

Na Mwandishi wetu

BAADHI ya Walimu Waratibu wa Vitengo vya Wanafunzi Walemavu vilivyopo katika shule za msingi Wilaya ya Arumeru wameiomba Serikali kuvisaidia vituo hivyo kifedha ili viweze kutekeleza programu zake anuai kwa lengo la kuboresha elimu kwa watu wenye ulemavu.

Wakizungumza katika mahojiano kwa nyakati tofauti hivi karibuni na mwandishi wa habari hizi kwenye vituo vyao, wamesema utaratibu wa wazazi kuchangia vituo hivyo umekuwa mgumu kwani wazazi/walezi wengi wa watoto walemavu wana uwezo mdogo kiuchumi.

Mratibu wa Kituo cha Walemavu cha Shule ya Msingi Iliboru, Loitusho Yamat alisema kitendo cha vituo hivyo kutokuwa na fungu maalumu hasa upande wa huduma ya chakula shuleni kimezifanya shule nyingi kutegemea wafadhili, watu ambao wanaweza kujiondoa muda wowote na vituo kuwa na hali mbaya.

“Unajua huduma ya chakula kwa wanafunzi walemavu ni muhimu zaidi, kwanza kundi hili haliwezi kuvumilia na kuendelea na masomo kama wana njaa…wakati mwingine wengine wanavutiwa na programu za chakula kisha anajikuta anapata na elimu…chakula ni muhimu kwa wanafunzi wa aina hii,” alisema Yamat.

Alisema tangu kituo hicho kianzishwe mwaka 2001 fedha ambayo Serikali imewekeza kihuduma haijafikia sh. 300,000; huku huduma ya chakula ikitolewa na mfadhili mmoja raia wa Marekani tangu 2005 hadi sasa.

Aidha Mkuu wa Kitengo cha Wanafunzi Walemavu cha Shule ya Msingi Naurei, Tuzie Mtenga alisema mbali na changamoto za kupungukiwa na vifaa vya kufundishia kama rangi, karatasi na vibao upande wa chakula kwa watoto limekuwa tatizo kwa vipindi tofauti.

Bi. Mtenga alisema chakula huwa wazazi husika wanachangia pamoja na wengine wanaoguswa na wanafunzi hawa, lakini wakati mwingine inakuwa ngumu kupata kutokana na wazazi wengi wa watoto wenye ulemavu kutokuwa na uwezo kiuchumi (kipato).

“Kwa mfano watoto wengi walemavu wengine wametelekezwa na wazazi wao kwa bibi zao, sasa watu hawa hawana uwezo sana wa kuchangia chakula ndiyo maana inakuwa tabu wakati mwingine kupatikana kwa huduma hiyo…sasa kama kungelikuwa na bajeti kutoka serikalini kupitia wizara husika hali ingelikuwa ni tofauti kidogo,” alisema.

Akizungumzia mwamko wa jamii kuhusiana na elimu kwa watoto wenye ulemavu eneo hilo amesema, kuna mafanikio kwani kikundi cha ‘Pambazuko Klabu’ kilichoanzishwa na shule hiyo kwa ushirikiano na Kituo cha Habari Kuhusu Ulemavu (ICD) kinaeneza kwa kutumia sanaa juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wenyeulemavu.

Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com kwa ushirikiano na Kituo cha Habari Kuhusu Ulemavu (ICD) cha jijini Dar es Salaam.  

No comments:

Post a Comment