Waandishi Wetu
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimewachochea walimu
wapya walioajiriwa hivi karibuni, warejee makwao iwapo Serikali itaendelea
kuwazungusha kuwalipa fedha za kujikimu pamoja na mishahara.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa (CWT), Gratian
Mukoba alisema wamepokea taarifa za malalamiko kutoka halmashauri mbalimbali
nchini kwamba walimu walioajiriwa Februari mwaka huu, hadi sasa hawajapata fedha
za kujikimu pamoja na mishahara.
“Sioni sababu ya walimu kuendelea kuteseka na kuwa
ombaomba wakati wapo kazini. Kama Serikali imeshindwa kuwalipa fedha zao za
kujikimu pamoja na mishahara wanatakiwa kurudi nyumbani kwao hadi itakapopata
fedha ndipo iwaite tena kazini,” alisema Mukoba.
Mukoba alisema kama hali itaendelea hivyo hadi mwisho
wa mwezi huu, CWT kitalazimika kuchukua hatua za kuhakikisha walimu wote
wanarudi nyumbani ili kuwaepusha na hali ya kuwatia majaribuni kutokana na
kuishi katika mazingira magumu.
“Napenda kuwaambia walimu ambao wataweza kuvumilia hali
hii hadi mwisho wa mwezi huu na kuona hakuna mabadiliko, nao wanatakiwa kurudi
kwao hadi pale Serikali itakapopata fedha. Hebu fikiria mwalimu hana sehemu ya
kulala, chakula nacho shida; halafu ananyimwa fedha zake. Unategemea nini?”
Alihoji Mukoba.
Alisema kitendo cha kuwalipa fedha za kujikimu za siku
tatu badala ya malipo ya siku saba ni ukiukwaji wa sheria za kazi na unyanyasaji
wa watumishi jambo ambalo CWT haitalivumilia.
Mukoba alisema malalamiko mengine ni ya fedha za madai
ya walimu ambayo yalihakikiwa na Serikali kati ya Novemba na Desemba lakini
ulipaji umegubikwa na utata.
“Kwa kweli unyanyasaji wa walimu umekithiri sana maana
hata walimu waliopo kazini kwa muda mrefu, fedha za madai ya zamani
yaliyohakikiwa na Serikali bado ulipaji wake ni utata mtupu. Walimu
wanazungushwa na kunyimwa fedha hizo lakini kwa sasa tunafikia hatua ya mwisho
ya kuchukua,” alisema Mukoba.
Kilio Kwimba
Taarifa kutoka wilayani Kwimba, Mwanza zinaeleza kuwa
walimu walioripoti mpaka sasa hawajalipwa fedha za kujikimu pamoja na
mishahara.
Mmoja wa walimu hao aliyelipigia simu katika ofisi za
gazeti hili alisema hivi sasa wana hali ngumu kwani walipewa fedha za kujikimu
kwa siku tatu tu tangu Februari 2 na hadi sasa wanaishi kwa
kuombaomba.
“Hapa tulipo hatuna fedha ya kula hata sehemu ya
kulala. Tatizo jingine ni kwamba hata uwezo wa kurudi kwetu hatuna maana hatuna
nauli na baadhi yetu, wazazi wetu hawana uwezo wa kututumia nauli turudi
nyumbani,” alisema.
Rungwe maandamano
Kutoka Rungwe mkoani Mbeya, walimu 206 wa shule za
msingi na sekondari jana waliandamana hadi Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wakidai
fedha zao za kujikimu, mishahara na nauli ambazo hawajalipwa tangu walipoajiriwa
mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Wakizungumza mbele ya ofisi hizo, walimu hao walisema
tangu waajiriwe walilipwa, fedha za kujikimu za siku tatu tu badala ya saba na
kwamba wamekuwa wakinyanyasika katika vituo vyao vya kazi.
Mmoja wao, Lucy Mpakati alisema wakati wanaripoti
waliahidiwa kwamba fedha zote zitakuwa zimelipwa mwishoni mwa Februari lakini
matokeo yake wanajikuta wanapigwa kalenda na mkurugenzi wa halmashauri...Soma
zaidi www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment