Waziri wa Mambo ya Ndani,Shamsi Vuai
Nahodha
ASEMA UCHUNGUZI BADO UNAENDELEA NA MATOKEO ATATANGAZA
YEYE, ATAKA MANUMBA AULIZWE MWENYEWE CHANZO CHA TAARIFA YAKE
Ramadhan Semtawa
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amesema
uchunguzi kuhusiana afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe bado
unaendelea na ni yeye atakayetangaza matokeo ya kama alipewa sumu au la baada ya
kukamilika huku akiikana ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa
ya Jinai (DCI) Kamishna, Robert Manumba.
Hii ni mara ya kwanza kwa Nahodha kutoa tamko hilo
tangu kuibuka kwa mjadala kuhusu afya ya Dk Mwakyembe hasa baada ya DCI Manumba
kuutangazia umma kwamba ripoti kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
inaonyesha kuwa Naibu Waziri huyo hakulishwa sumu, kauli ambayo ilipingwa na
Waziri mwenye dhamana ya Afya, Dk Haji Mponda na Dk Mwakyembe
mwenyewe.
Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar
es Salaam jana, Nahodha alisema uchunguzi kuhusu afya ya Dk Mwakyembe ni wa
kisayansi na hauwezi kufanyika ndani ya wiki mbili au mwezi.
“Ninachosema ni kwamba uchunguzi nilioutangaza bado
unaendelea,” alisema na kuongeza: Sasa mimi nimetangaza matokeo ya uchunguzi?
Mimi ndiyo Waziri nasema uchunguzi bado unaendelea na mimi ndiyo nitatangaza
hitimisho la jambo hilo.”
Alisema suala la Dk Mwakyembe ni zito na siyo la mtu
kukurupuka kwani linagusa hisia za watu na kutahadharisha baadhi ya watu
wanaojaribu kulifanya jepesi wanachezea kitu hatari.
“Ndiyo maana nasema ni jambo linalohitaji weledi wa
hali ya juu katika kulichunguza. Ni jambo zito la kisayansi, naomba nipewe muda
ili uchunguzi nilioagiza ufanyike kwa kina. Nasisitiza ni jambo linalohitaji
weledi wa kisayansi.”
Waziri Nahodha alisema uchunguzi huo unafanyika kwa
kuhusisha jopo la wataalamu wa sayansi hivyo kuwataka Watanzania kutambua kwamba
uchunguzi huo unaendelea na ni vigumu kutamka utakamilika lini.
Kuhusu ripoti ya DCI
Alipoulizwa ni kwa nini asimchukulie DCI Manumba hatua
kwa kutoa tamko wakati uchunguzi alioagiza haujakamilika alisema: “Ndiyo maana
nasema, uchunguzi wa suala hili unaendelea. Sasa hatima yote hayo unayozungumza
nasema nipeni muda.”
Alipoulizwa ni wapi DCI Manumba alipata ripoti ya Dk
Mwakyembe wakati mgonjwa mwenyewe na Waziri wa Afya wameikana, alijibu: “Sasa,
hilo ni vyema ukamtafuta yeye mwenyewe DCI aseme. Mtafute aseme yeye na Waziri
wa Afya, hao watu wawili wanaweza kuzungumzia ripoti hiyo, lakini mimi nasema
uchunguzi wa jambo hili la Dk Mwakyembe ni wa kisayansi na bado
unaendelea.”
Alisema alichokisema DCI Manumba kinaweza kuwa na
msingi ambao anaujua mwenyewe hivyo, ni vyema akaulizwa yeye kuhusu undani wa
ripoti yake huku akisisitiza: "Mimi ninavyoliangalia jambo hili la Dk Mwakyembe
linahitaji umakini wa hali ya juu katika kulishughulikia. Hilo la DCI mtafute
mwenyewe akueleze.”
Nahodha pia hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani
hata pale alipoulizwa ikiwa haoni kwamba kukanwa kwa kiwango hicho kikubwa kwa
ripoti ya DCI Manumba kunawafanya wananchi waanze kutilia shaka utendaji kazi wa
jeshi la polisi.
Hata hivyo, alipoulizwa jana kuhusu kukanwa kwa ripoti
yake na mawaziri, akiwemo wa Mambo ya Ndani ambayo ndiyo wizara mama
inayosimamia Jeshi la Polisi, DCI Manumba alisema kimsingi hawezi kujibizana na
waziri yeyote kwani kufanya hivyo itakuwa ni utovu wa nidhamu katika utumishi wa
umma.
Alisema alichokifanya ni kuandaa jalada ambalo tayari
liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye kwa mamlaka na utaalamu wake wa
kisheria, ataamua cha kufanya baada ya kulipitia.
“Siwezi kujibizana na waziri wangu au waziri yeyote.
Kama amesema uniulize mimi, ninachoweza kusema ni kwamba tayari nimeandaa jalada
liko kwa DPP. Sasa nikianza kuzungumza hili au lile itakua haina maana watu
watasema nimeanza kujitetea,” alisema.
DCI, Dk Mwakyembe na Dk Mponda
Akizungumza na waandishi wiki mbili zilizopita, DCI
Manumba alisema: “Ukweli kuhusu kauli hiyo inayodai kuwekewa sumu, tumeupata
baada ya kuwasiliana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambayo nayo
imewasiliana na hospitali aliyokuwa amelazwa Dk Mwakyembe nchini India. Taarifa
zinaonyesha kuwa hakuna sumu.”
“Hatua zaidi zinachukuliwa dhidi ya jambo hilo, kwa
sasa litashughulikiwa kwa kufuata misingi ya kisheria,” alisema
Manumba.
Hata hivyo, siku moja baada ya kauli hiyo ya DCI
Manumba, Dk Mwakyembe alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema: "Napata tabu
kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu
au walisoma taarifa ‘nyingine’ na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au
‘walisomewa!’
“Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa
waandishi wa habari, hakifanani kabisa na picha iliyoko kwenye taarifa halisi ya
Hospitali ya Apollo inayotamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow (uboho)
kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua,
kukidhibiti au kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi
kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “Hakulishwa sumu”, “hakulishwa
sumu.”
Dk Mwakyembe pia alitoa sababu kuu tatu za kupinga
ripoti ya DCI Manumba: “Kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na
uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake, unaoendelea katika Hospitali ya Apollo,
India ambako bado sijahitimisha matibabu yangu, pili kwa ufinyu wa uelewa
unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa
‘sikunyweshwa sumu’ wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza
kudhuru hata kwa kugusishwa tu.
Soma zaidi www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment