Mhashamu Telesphor Mkude,
Askofu wa jimbo la Morogoro
PADRI wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Lugoba Jimbo la
Morogoro, Philipo Mkude amezuiwa na waumini kuongoza misa baada ya kudaiwa
kuwakashifu waumini wa kabila la Wakwere.
Padri Mkude alizuiwa kuongoza misa jana asubuhi
parokiani hapo, baada ya waumini zaidi ya 200 kuandamana wakiwa na mabango zaidi
ya 20 wakidai ahamishwe kwa kuwa amewatukana katika mahubiri yake, kwamba watoto
wao ni wachafu na wao wamebaki kucheza ngoma badala ya kufanya
maendeleo.
“Tumechoka na mahubiri ya huyu Padri, kila akihubiri
kanisani lazima atuseme Wakwere,
tumemkosea nini?
Mara atuseme tu masikini, mara watoto wetu wachafu na
hatuwapeleki shule tunashindia ngoma, tumechoka, hatumtaki,” alisema muumini
ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
“Leo tumemzuia asisome misa kabisa, hakuna haja maana
hakuna amani kanisani, hatujui ana kitu gani na sisi, sijui kwa sababu parokia
hii ipo kwa Wakwere?
“Hata Jumatano ya Majivu wiki iliyopita katusema tena,
eti watoto wetu ni wachafu sana ukilinganisha na makabila mengine, hii ni
kashfa.”
Wakwere ni moja ya makabila katika Mkoa wa Pwani
linalopatikana wilayani Bagamoyo,
lakini katika mfumo wa Kanisa Katoliki, Parokia ya
Lugoba ipo chini ya Jimbo la Morogoro.
Muumini huyo aliyezungumza kwa simu na mtandao huu wa kijamii alisema kuwa mahubiri ya Padri huyo ya kuwasema Wakwere hayakuanza siku za
karibuni, bali ni ya muda mrefu na yamekuwa kama ya kusutwa badala ya kulishwa
Neno la Mungu.
“Hali hiyo imesababisha watu kutokwenda kanisani
wakijua leo Padri huyo anaongoza misa, lakini akiongoza Katekista, misa inajaa
utadhani Askofu amekuja, tunachotaka hapa ni Padri mwingine, kama Askofu
anatujali atuletee mwingine,” alisema muumini huyo.
Kwa mujibu wa muumini huyo, walifanya maandamano ya
amani kuanzia saa moja asubuhi kabla ya misa iliyopaswa kuanza saa 2.30 asubuhi
huku wakiimba nyimbo za dini na mabango yenye ujumbe mbalimbali ukionesha kauli
tofauti za padri huyo na namna walivyomchoka.
Alidai pia hali hiyo ilisababisha misa isifanyike baada
ya Polisi pamoja na Diwani wa Msoga,
Mohamed Mzimba kufika kanisani hapo na kumshauri Padri
huyo aondoke eneo hilo na kwenda Parokia ya jirani ya Chalinze umbali wa
kilometa 22 ili kurejesha amani eneo hilo.
Diwani Mzimba alipoulizwa alikiri na kusema; “nilifika
hapo nilipopewa taarifa kwamba hali si
shwari, mimi si wa Kata ya Lugoba, lakini mwenzangu
anaumwa…kweli wameandamana,
lakini kwa amani na wana madai yao.”
“Ujumbe wameutoa kwa mabango, mengine yaliandikwa
hatumtaki kapoteza kikombe chetu
cha dhahabu cha divai na mengine anatukana Wakwere,
mimi si Mkristo sasa sijui zaidi, ila kuondoa jazba waliyokuwa nayo, Polisi
walimshauri Padri aende kanisa la Chalinze huku viongozi wa kanisa wakimaliza
mzozo,” alisema Mzimba.
Katekista (Mwalimu wa Mafundisho wa Dini) wa Parokia
hiyo, Prosper Semindu alipoulizwa
kuhusu tukio hilo, alikiri kutokea na kueleza kuwa
haelewi sababu ni nini ila waumini hao walikuwa na mabango huku wakiimba nje ya
kanisa na kusababisha misa isifanyike.
Padri Mkude alonga
Padri Mkude alipoulizwa jana alikana kuwatukana na
badala yake alidai kuwa katika mahubiri yake amekuwa akiwasisitiza kusoma kama
ambavyo viongozi kadhaa, akiwemo Rais Jakaya Kikwete amekuwa
akiwaeleza.
“Watu kuwasema Wakwere kuhusu elimu ipo tangu zamani,
nilikuwa nawasisitiza hata
wachimbe vyoo, hawataki, wanauza mashamba ambayo ni
urithi kwa watoto, niliwaambia
jamani msiuze mtashindwa kusomesha watoto, hawanisikii,
wanabaki kucheza ngoma, sasa
nimewatukana wapi?
“Jumatano ya Majivu niliwaambia wabadilike hasa kuhusu
elimu, kwamba tufanye bidii katika shule yetu hapa Lugoba kidato cha nne wapo
wanafunzi 250 kutoka Pwani, angalau 70 waende kidato cha tano na tukipata watoto
angalau 10 vyuo vikuu miaka 10 ijayo tutakuwa na
wasomi wengi, leo wanasema unatunyanyasa na
kututukana,” alisema Padri Mkude.
Alisema alipoona maandamano aliwaeleza kuwa kama
amefanya makosa ya jinai watoe taarifa kwa vyombo vya usalama na kama ni makosa
ya kikanisa, wafikishe mahali husika, lakini si kuvamia ibada na kufanya
maandamano bila ruhusa.
Walivyoanzisha vurugu
Akielezea hali ilivyokuwa, Padri Mkude alisema wakati
akijiandaa kuanza ibada baada ya kengele ya kwanza na ya pili kulia, muumini
mmoja alimfuata kumsalimu na kisha alimwambia hawataki aongoze Misa na kama
akifanya, hakutakuwa na usalama kwenye Misa.
“Wakati huo tofauti na siku nyingine, hakukuwa na mtu
kanisani, niliwauliza kwa nini,
wakasisitiza niondoke, huko nje walikuwa wengi
wanaimba, nikawaambia kama mmekataa misa, basi.
Viongozi wa Baraza la Walei walitoa taarifa Polisi,
wakaja na mimi nikaondoka,” alisema Padri Mkude.
Alisema hivi sasa yupo Parokia ya Chalinze na anasubiri
uamuzi wa kikao kati ya Ujumbe wa Askofu wa Morogoro na kundi la waumini hao ili
kumaliza suala hilo. Mpaka jana jioni, kikao hicho kilikuwa
kikiendelea.
No comments:
Post a Comment