Naomba nichangie kuhusu hili suala la shule za kata na
ukosefu wa walimu. Binafsi ninayo maoni tofauti na wengi wanaozibeza kwamba ni
mzigo na hazina tija hata kidogo katika maendeleo ya elimu
Tanzania.
Kusema ukweli wengi tunakumbuka enzi zile ambazo
kulikuwa kuna uhaba wa shule za sekondari kiasi kufaulu darasa la saba ilikuwa
ni ndoto za alinacha. Kwa vile wakati ule shule za sekondari hazikuwa nyingi nap
engine kila mkoa ulikuwa na walau shule moja au mbili, na kulikuwa na shule zile
za kitaifa zilizochukuwa wanafunzi kutoka kila kona ya nchi. Hapo utataja shule
za Mazengo, Mkwawa, Ilboru, Msalato, Tabora Girls, Tabora Boys na Mzumbe kutaja
chache.
Nafikiri ni kwa kutambua uhaba wa shule za sekondari za
kutosha na pia ile hamu kubwa ya kukata kiu ya kupata elimu kwa kila mtanzania
ndio serikali yetu ikaja na mpango wa kupanua elimu kwa kuongeza idadi ya shule
kwa kuanza na mpango wa shule za msingi na baadae kufuatia na ule mpango wa
shule za sekondari.
Kwa bahati mbaya katika utekelezaji wa mipango yote
hiyo kumekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa walimu na vifaa vya kufundishia
kwa ngazi zote. Na kutokana na hili ndio maana watu wengi wamekuwa wakikashifu
na hata kutoa kejeli kwa mpango mzima ambao mbali na mapungufu hayo umekuwa na
mafanikio ya wastani lakini ambayo ninayo matumaini yatakuwa
endelevu.
Kwanza kabisa ni dhahiri kumekuwa na ongezeko la idadi
ya wanafunzi wanaojiunga na sekondari tangu kuanzishwa kwa mpango huu. Na hapa
wengi wanakosoa kwamba hili halina tija kwa kuwa kwa changamoto zilizopo katika
shule zinafanya elimu itolewayo kuwa ya chini na isiyo na tija. Katika hili
sipangani na wanaotoa kasoro hizi ingawa naamini bado hata katika hilo kundi la
shule za kata wapo baadhi ya watoto wetu wanaofaulu na kuendelea mbele na elimu
za juu, tofauti na namna ilivyokuwa zamani wakati ambapo hata upenyo wa kuingia
kwenye mfumo wa elimu haukuwepo.
Baada ya kujaribu kutoa hayo maelezo machache sasa
naomba nieleze jambo moja ambalo mimi nafikiri linaweza kusaidia kupunguza
changamoto ya ukosefu wa walimu katika hizi shule. Nimejaribu kupitia mfumo wa
ukopeshwaji wa miko[o kwa ajili ya elimu ya juu na suala la kujiunga na mfumo wa
Jeshi la Kujenga Taifa (National Service) na hapa ndio nikaona kuna mwanya wa
kupata suluhu ya tatizo hili. Nionavyo mimi serikali inapaswa iandae mpango
ambao utwalazimisha wanafunzi wanaohitimu katika vyuo mbalimbali nchini kwenda
kufundisha katika hizi shule za kata kwa walau kipindi cha mwaka
mmoja.
Kwa kufanya hivi serikali itatakiwa kuwapa posho za
kujikimu wahitimu hawa na kwa kiasi fulani cha mshahara, kiasi kinaweza kukatwa
kufidia mkopo ambao wahaitimu walikopeshwa na serikali kugharamia elimu za chuo
kikuu.
Wapo wanaoweza kuona mpango huu hauna mantiki, lakini
kiukweli katika wakati tulionao hatuna suluhisho la haraka na la unafuu kama
hili. Wanaweza kuja wasemaji, kwamba wahitimu hao hawatakuwa na weledi wa
kiualimu, lakini jawabu ni kwamba katika Tanzania tumekuwa na programu nyingi za
kuwapika walimu kwa muda na baadhi zimeweza kutoa walimu ambao wengi tumepitia
kwao. Tunakumbuka mpango wa UPE, Mama Sita Programe (VODA FASTA)
nk.
Lakini mbali na hilo serikali pia itatatua kwa kiasi
tatizo la wahitimu wa vyuo vikuu kukwepa kulipa mikopo baada ya
kuhitimu.
Ili kutekeleza na kusimamia mpango huu serikali
inapaswa kuwa na mpango wa kutoa vyeti maalumu vitakavyotolewa kwa wale
watakaomaliza vyema muda wao kufundisha na hicho ndio kiwe kibali kwa taasisi
kumuajiri mhitimu wa chuo.
Najua viongozi wetu wanao nafasi ya kujifunza zaidi
namna bora ya utekelezaji wa mpango na mipango zaidi ya kukwamua sekata ya elimu
na nyinginezo, kwa hiyo kwa kujifunza zaidi namna ya utekelezaji wanaweza
kujifunza katika nchi ya Ghana namna hizi programu zinavyoendeshwa.
Naomba kuwakilisha
No comments:
Post a Comment