ANIKA ALIVYOSHIRIKI KATIKA MCHAKATO KIPINDI AKIWA
WAZIRI MAMBO YA NJE, ASEMA ALIKUTANA NA MAMA MWENYE NYUMBA NA KUAGIZA ALIPWE
DOLA MILIONI MOJA HARAKA, AKAMPA OFA KUJA MBUGA YA NGORONGORO
Tausi Ally
ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa
Costa Mahalu ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Rais Jakaya Kikwete
wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alifahamu
kuwepo kwa rasimu mbili za mikataba ya ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania,
Italia.
Profesa Mahalu alisema hayo jana mbele ya Hakimu
Mfawidhi, Ilvin Mgeta wakati akitoa utetezi wake dhidi ya kesi inayomkabili ya
uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 pamoja na
aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin.
Akiongozwa na wakili wake, Mabere Marando, Profesa
Mahalu aliitambua barua ya Februari 20, 2002 ambayo ilikuwa ikieleza kuwa
matayarisho yote ya ununuzi wa jengo la ubalozi huko Italia yamekamilika ikiwa
ni pamoja na rasimu mbili za mikataba.
Mahalu alidai kuwa katika mchakato wa ununuzi wa jengo
hilo wakati yeye akiwa Balozi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, kulikuwa na rasimu mbili za mikataba na kwamba aliwahi kuwasiliana na
wizara hiyo juu ya mikataba hiyo.
Alidai kuwa Desemba 2001, Kikwete wakati huo akiwa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alikwenda Rome, Italia kwenye
Mkutano wa SADC na alipokuwa huko, ubalozi ulifanya mpango atembelee jengo hilo
lililopendekezwa kununuliwa kwa ajili ya ofisi ya ubalozi.
“Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia ilifanya mipango yote
kwa kumpa utaratibu na usalama Kikwete ambapo alikwenda kutembelea jengo hilo na
kukutana na mama mwenye jengo,” alidai Profesa Mahalu.
Alidai kuwa kabla ya mazungumzo na mwenye nyumba, mtoto
wa mama huyo, Alberto alimtembeza Kikwete kwenye jengo hilo ndani na nje na
baadaye mazungumzo hayo yaliendelea.
Balozi Mahalu alisema baadaye mazungumzo kati ya
Kikwete na mama huyo yaliendelea na Alberto alikuwa akitafsiri, kwa sababu mama
yake hakufahamu lugha ya Kiingereza.
Profesa Mahalu alidai kuwa katika mazungumzo hayo,
Kikwete alimwuliza mama huyo: “Hivi ni kwa nini kunakuwa na mikataba miwili?” na
mama huyo alimjibu kuwa hiyo ni kawaida kwa Italia ukitaka kununua jengo kwa bei
nafuu.
Profesa Mahalu aliendelea kudai kuwa baada ya kupewa
jibu hilo, Kikwete hakuzungumza tena zaidi ya kucheka na kwamba mwenye jengo
alimkumbusha kuhusu malipo ya awali ya dola milioni moja za Marekani ambapo
aliafiki na kuahidi kuwa zingelipwa kabla ya mwisho wa mwaka 2001.
Profesa Mahalu alidai pia kwamba Kikwete alimweleza
mama huyo kuwa atalishughulikia suala hilo baada ya kurejea Dar es Salaam na
kumshukuru kwa kuwauzia jengo zuri.
Baada ya kutoa maelezo hayo, Profesa Mahalu alidai kuwa
baada ya Kikwete kusema maneno hayo, alimgeukia na kumwambia: “Costa ni vizuri
tupate hela tumlipe huyu mama watu wengine wasije wakachukua hili
jengo.”
Profesa Mahalu alidai kuwa baada ya Kikwete kumshukuru
mama huyo kwa ukarimu wake, alimkaribisha Tanzania awe mgeni wa Wizara ya Mambo
ya Nje yeye na mumewe na kwamba watampeleka Ngorongoro.
“Tulipokuwa njiani tukirudi hotelini alipofikia Kikwete
akiwa kwenye gari alimpigia simu Kibero akimuagiza afanye utaratibu wa kulipa
Dola milioni moja kama malipo ya awali ya jengo hilo,” alidai Profesa
Mahalu.
Alidai kuwa baadaye alimwagiza (Profesa Mahalu) aje Dar
es Salaam kufuatilia mpango huo wa malipo ya awali ya ununuzi wa jengo
hilo.
Awali, Profesa Mahalu akiongozwa na Wakili Alex
Mgongolwa alidai kuwa anaitambua ripoti ya uthamini wa jengo hilo la ubalozi
nchini Italia uliofanywa na Kimweri kutoka Wizara ya Ujenzi aliyekwenda Rome
Julai 15 hadi 26, 2001 kwamba jengo lilikuwa na gharama ya Sh6
bilioni.
Soma zaidi www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment