• Kisa ni kifo cha ghafla cha mhudumu ofisini
kwake
WARAKA wa siri ulioandikwa na Naibu Waziri wa Ujenzi,
Dk. Harrison Mwakyembe, umezidi kuibua mambo mapya.
Waraka huo ulioripotiwa mara ya kwanza wiki iliyopita
na gazeti hili na kueleza mbinu, mahala ambapo waziri huyo anaamini aliwekewa
sumu kupitia sabuni na taulo vilivyowekwa ofisini kwake kwenye chumba cha
kuoshea mikono, safari hii waraka huo unaendelea kwa kumtaja mhudumu aliyetumika
kuweka vitu hivyo.
Kupitia waraka huo alioutoa kwa ndugu na rafiki zake wa
karibu, Dk. Mwakyembe anasema mhudumu aliyetumika bila kujijua ni wa kike kutoka
katika kijiji cha Ipinda, wilayani Kyela, mkoani Mbeya, ambaye alihamishiwa
ofisini kwake.
Inaelezwa kuwa mhudumu huyo aliletwa katika ofisi hiyo
siku chache kabla ya siku ya kuweka sabuni na taulo jipya ofisini kwa waziri
huyo.
“Nilipoona kuwa najikuna mfululizo mara baada ya
kunawia sabuni hiyo, siku ya tatu nilikuwa na wazo la kupeleka vitu hivyo kwa
Mkemia Mkuu wa Serikali, lakini nilipofika ofisini, vilikuwa vimeshatolewa,”
anasema Dk. Mwakyembe kupitia waraka huo.
Dk. Mwakyembe ambaye yuko nchini India kwa awamu ya
pili ya matibabu, anasema alianza kumuuliza maswali ya kina mhudumu huyo ili
kujua kwa nini vifaa hivyo viliondolewa ghafla wakati alivitumia siku moja,
hakufanikiwa kupata majibu ya kina.
Naibu waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, anadai
katika mazingira ya kutatanisha, tena ndani ya muda mfupi tangu alipoanza
kuathirika baada ya kunawia sabuni na kujifutia taulo hilo, mhudumu huyo wa kike
alifariki na kuzikwa kijijini kwao Ipinda.
Tukio la kufariki ghafla kwa mhudumu huyo bila kuugua,
limeacha maswali mengi sio tu kwa Dk. Mwakyembe, bali pia hata kwa rafiki zake
wa karibu ambao wanaamini kwamba aliwekewa sumu.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na gazeti hili
kuhusiana na taarifa kwamba kuna mhudumu mmoja wa kike wa Dk. Mwakyembe
alifariki zilithibitisha kuwa ni kweli.
Mmoja maafisa wa juu wa wizara hiyo, aliliambia
Tanzania Daima Jumatano kwa sharti la kutotaja jina lake kuwa ni kweli mhudumu
huyo aliyemtaja kwa jina moja la Sara Richard ambaye alikuwa akimsadia Naibu
Waziri huyo alifariki Septemba 29, mwaka jana, na kuzikwa kijijini kwao
Ipinda.
“Ni kweli kuna mhudumu mmoja ofisini kwa Dk. Mwakyembe
alifariki mwaka jana. Ila sijui aliugua ghafla au vipi hilo sijui; isipokuwa ni
kweli kwamba mwaka jana tulimpoteza mtumishi mmoja na tulimsafirisha hadi kwao
Mbeya,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Akihojiwa na gazeti hili kuzungumzia waraka huo na
tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, alisema hajauona na
kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa
jambo hili.
Hadi sasa wingu zito limetanda kuhusu afya ya Dk.
Mwakyembe.
Wakati taarifa zisizo rasmi zikisema amepewa sumu,
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI), Robert Manumba, amesema hajalishwa
sumu...Soma zaidi www.freemedia.co.tz
No comments:
Post a Comment