MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imempanga Jaji Laurence
Kaduri kusikiliza maombi ya marejeo ya mwenendo wa kesi ya ugaidi
inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred
Lwakatare na mwenzake, Ludovick Joseph.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya mawakili wanaomtetea Lwakatare
kuwasilisha maombi ya marejeo ya mwenendo wa kesi hiyo, iliyofunguliwa
katika Mahakama ya Kisutu.
Maombi hayo ya marejeo yaliwasilishwa mahakamani hapo chini ya hati ya
dharura yakiambatanishwa na hati kiapo ya mmoja wa mawakili wanaomtetea
Lwakatare, Peter Kibatala.
Mawakili wengine katika jopo hilo la utetezi ni Mabere Marando, Profesa Abdallah Safari, Nyaronyo Kicheere na Tundu Lissu.
Chanzo chetu kutoka mahakama kuu, kilisema kuwa pamoja na Jaji Kaduri
kupangiwa kusikiliza maombi hayo, bado tarehe rasmi haikutajwa kutokana
na majaji kuwa kwenye likizo fupi ya sikuu za Pasaka.
“Mahakama itaanza tena shughuli zake Aprili 2, hivyo kuanzia tarehe hiyo maombi hayo yatasikilizwa,” alisema mtoa taarifa.
Tayari Makahakama Kuu ilikwishatoa hati ya kuitisha majalada hayo iliyotolewa na Msajili wa Mahakama hiyo.
Wiki iliyopita mawakili wanaomtetea Lwakatare waliwasilisha maombi
hayo ambayo yalipokelewa na kupewa usajili wa namba 14 ya 2013.
Mawakili hao waliiomba Mahakama Kuu, iitishe majalada yote mawili ya
kesi hiyo, jalada namba 37 ya mwaka 2013 na namba 6 ya mwaka 2013 kwa
ajili ya uchunguzi ili iweze kujiridhisha usahihi na uhalali wa mwenendo
wake.
Pia wanaiomba Mahakama Kuu ifanye marejeo au kutengeua hati ya
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iliyowafutia mashtaka watoa maombi kabla ya
kuwakamata na kuwafungulia tena mashtaka hayo hayo.
Maombi yao mengine ni kutaka Mahakama ya Kisutu iamriwe kutoa uamuzi
wa maombi ya dhamana, uliokuwa umepangwa kutolewa na Hakimu Mkazi
Mwandamizi, Emillius Mchauru, Machi 20, 2013, katika kesi namba 37.
Mawakili hao wanadai kuwa uamuzi huo ambao ulihusu dhamana ya
watuhumiwa, ulitenguliwa na hati ya DPP ya kuwafutia mashtaka washtakiwa
hao, isivyo halali.
Maombi mengine ni kurejea au kutengua mwenendo wa kesi namba 6
iliyofunguliwa baada ya hati ya kuwafutia mashtaka watoa maombi hao na
badala yake iendelee kesi namba 37.
No comments:
Post a Comment