Monday, October 8, 2012

DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO MAALUM WA WAKUU WA NCHI ZA MAZIWA MAKUU, KAMPALA UGANDA

Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amemuwakilisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika mkutano maalum wa wakuu wa nchi za Maziwa Makuu mjini Kampala Uganda leo Oktoba 08, 2012. Mkutano huu maalum una agenda moja kubwa ambayo ni kujadili na kisha kupitisha maamuzi kuhusu mustakhbali wa hali ya usalama wa kudumu katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo.
Mheshimiwa Makamu wa Rais na ujumbe wake umewasili nchini hapa salama na moja kwa moja kushiriki kupata taarifa za mikutano ya ngazi ya Mawaziri ambapo Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Omari Juma Mahadhi. Katika mazungumzo hayo ya awali, Mheshimiwa Waziri Vuai alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, Tanzania inabakia kuwa na sifa yake ya siku zote ya kuthamini na kujitoa kusaidia kupatikana kwa amani katika nchi zinazoizunguka sambamba na zile zinazohitaji msaada wake. Akifafanua kuhusu makubaliano katika ngazi ya Mawaziri, Waziri Vuai alimhakikishia Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa Tanzania imewakilishwa vizuri na kwamba nchi nyingine wanachama zinategemea sana mchango wa Tanzania katika kuisaidia Congo (DRC) kufikia amani ya kudumu na hivyo wananchi wake kuendelea na shughuli za kunyanyua vipato vyao bila hofu ya usalama wa maisha yao.

Kwa upande wake Mheshimiwa Naibu Waziri Mahadhi alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuhusu ushiriki wa Tanzania katika nchi za Maziwa Makuu na akafafanua kuwa nchi hizi zinategemeana sana katika hali mbalimbali za maisha hivyo Tanzania bado inayo fursa nzuri ya kuendeleza mahusiano na nchi hizi kwa angalizo kubwa la kutazama fursa za kiuchumi.

No comments:

Post a Comment