Friday, June 1, 2012

Benjamin Mkapa afunguka



RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, jana alisema kwa sasa hataki kusumbuliwa kwa namna yoyote, badala yake ameomba aachwe huru ili ashughulikie matatizo aliyonayo.

Bila kutaja aina ya matatizo hayo, Mkapa alikataa kuzungumza na waandishi wa habari akidai kuwa hataki kuongeza matatizo mengine, kwa vile aliyonayo kwa sasa yanamtosha.

Mkapa alitoa kauli hiyo baada ya kuombwa na kundi la waandishi wa habari mara baada ya kutoka kwenye mjadala maalumu kuhusu uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji barani Afrika, ulioandaliwa na Taasisi ya Uwezeshaji na Uwekezaji (ICF).

Waandishi walitaka kufanya mahojiano na Rais huyo mstaafu kuhusiana na mambo kadhaa yakiwemo aliyozungumza katika mkutano huo, ambayo yalikuwa mazito na ‘mwiba’ kwa watawala wengi wa serikali barani Afrika.

“Niacheni, nina matatizo yangu ya kunitosha, sitaki kuongea kwa sasa,” alisema na kisha akaondoka.

Rais Mkapa amekuwa akishambuliwa na viongozi mbalimbali wa siasa kwa madai ya kuuza mashirika ya umma, kutumia wadhifa wake na kujimilikisha kampuni ya uchimbaji madini, akishirikiana na baadhi ya waliokuwa mawaziri katika serikali yake.

Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakipendekeza Rais huyo wa zamani akamatwe kwa kuhusika na tuhuma za ufisadi, kama ilivyofanywa kwa baadhi ya mawaziri wake wa zamani kwa tuhuma za ubadhirifu.

Mkapa aliingia hivi karibuni katika mzozo mzito na familia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, baada ya kukaririwa akisema Mbunge wa Musoma, Vicent Nyerere (CHADEMA), hakuwa mtoto wa Mwalimu, kauli aliyoitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki, wakati akimnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari.

Mapema akizungumza katika mjadala uliohudhuriwa na washiriki toka makampuni na taasisi mbalimbali za bara la Afrika, Mkapa alisema alifanikiwa wakati wa utawala wake kutokana na sera yake ya uwazi na ukweli, na pia kujikita katika utekelezaji wa mipango.

Alisema sio vema kwa viongozi wa nchi za Afrika kuzungumzia mipango na mikakati ya maendeleo kila kukicha, badala yake waingie kwenye utekelezaji.

Alisema kuwa sera yake ya uwazi na ukweli ilisaidia kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu hali ya uchumi, fedha na changamoto zote zilizoikabili serikali na wao kupata fursa ya kushiriki kuzitafutia ufumbuzi.

Mkapa alisisitiza umuhimu wa serikali za Afrika kuwawezesha kiuchumi wanawake na vijana waweze kujiajiri kwa kuwa hayo ndio makundi makubwa kuliko makundi mengine katika jamii hivyo itaziwezesha nchi hizo kupiga hatua za kimaendeleo kwa haraka na kukabiliana na tatizo la umaskini wa kipato.

Alisema kuwa tatizo la ajira limesababisha vijana wengi kughiribiwa na wanasiasa ambao huwapa matumani hewa ya mafanikio, na wengi kuamini kuwa njia sahihi ya kujinanusa ni kujiingiza katika siasa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ICF, Omary Issa, alisema taasisi hiyo imefanikiwa kuboresha mifumo mbalimbali inayopunguza usumbufu kwa wafanyabiashara na wawekezaji huku akitolea mfano wa mpango wa kuboresha mfumo wa usafirishaji mizigo toka bandarini mpaka nchi jirani wanaoutekeleza kwa pamoja na mamlaka ya mapato nchini TRA na Jeshi la Polisi ambao utawezesha kuondoa vizuizi vyote vya kodi barabarani.

Alisema kuwa ICF imesaidia kuboresha mfumo wa usajili wa makampuni nchini Rwanda ambapo kwa sasa huchukua siku 2 kusajili biashara tofauti na awali ambapo ilikuwa mpaka siku 16 huku gharama zikipungua kutoka dola za Marekani 433 mpaka 25.

Issa alisema kuwa taasisi yake katika kuhakikisha shughuli za biashara zinafanyika kwa urahisi na ufanisi zaidi imesaidia kuboresha mfumo wa mahakama nchini Zambia kwenye mahakama tatu na kutoa mafunzo kwa majaji wapya 14 huku nchini Sierra Leone wakifanikiwa kuboresha mfumo wa mahakama ambapo kwa sasa huchukua miezi miwili tokea kufungua kesi za biashara na kupata uamuzi ambapo awali ilikuwa inatumia mpaka miaka sita.

No comments:

Post a Comment