Wednesday, March 7, 2012

WAZIRI MAGUFULI AMTAHADHARISHA MKANDARASI ANAYEJENGA BARABARA YA MSATA - BAGAMOYO


 









Na Mwandishi wetu
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Bagamoyo hadi Msata ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi Estim Construction Company Ltd.
Katika ziara hiyo Mhe. Magufuli aliandamana na wataalamu mbali mbali kutoka Wizara ya Ujenzi Makao Makuu na Tanroads. Msafara huo hata hivyo ulilazimika kufanya kikao cha dharura eneo la Kiwangwa ambako ndipo sehemu ya lami kuanzia Msata ilipoishia ikiwa na urefu wa kilometa 25 tu kati ya kilometa 64 zinazokusudiwa kujengwa kwa mradi wote..
Mhe. Magufuli alielezea kuridhishwa na kiwango cha ujenzi alichokiona na kumtaka mkandarasi huyo kuendelea kuzingatia viwango hivyo alivyowekewa kimkataba. Hata hivyo wakati akipokea taarifa ya mradi alishtushwa kubaini kuwa hadi sasa mkandarasi huyo ametekeleza asilimia 46 tu ya kazi zilizopangwa wakati ambapo amekwishatumia asilimia 73 ya muda wa mradi wote.
Akitoa ufafanuzi Mwakilishi wa Kampuni ya JBG Gauff Ingenieure GMBH & CO ambayo ndiyo inayomsimamia mkandarasi wa mradi huu Injinia Kini Kiyoniza, alielezea kuwepo kwa ongezeko kubwa la viwango vya kazi kwamba ndiyo sababu ya kuchelewa kwa utekelezaji.Maelezo haya hayakumridhisha Waziri Magufuli na akamuagiza Mtendaji Mkuu wa Tanroads kuhakikisha anausimamia kwa karibu mradi huu na kuhakikisha kuwa hakuna visingizio vitakavyotolewa na kusababisha ongezeko la muda au gharama za mradi huu.
Ilielezwa kuwa Mkandarasi huyo anatakiwa kuwa amekamilisha mradi huu ifikapo mwezi Septemba mwaka huu wa 2012, za zipo kila dalili kuwa hataweza kumaliza kwa muda uliobaki kitu kilicho mlazimu Waziri Magufuli kuhoji ni kwanini mkandarasi huyo asijigawe katika makundi mawili kwani anavyo vifaa na kwamba hata madai yake yote yamelipwa kwa asilimia 100 hivyo kutokuwa na visingizio vyovyote vya ucheleweshaji.
Akimalizia Waziri wa Ujenzi alimtahadharisha Mkandarasi Estim kwamba Serikali haitakuwa tayari kuendelea kutoa kazi nyingine kwa makandarasi ambao wanashindwa kukamilisha kazi walizo nazo hadi wazikamilishe.
Alifafanua kuwa lengo ni kuwakuza makandarasi wazalendo lakini nao ni lazima waonyeshe kuwa wanauwezo wa kutekeleza kazi wanazopewa kwa ufanisi kwani miradi hii hutumia fedha nyingi za walipa kodi na hivyo ni budi zisimamiwe ipasavyo.Mradi wa ujenzi wa barabara kati ya Bagamoyo na Msata utagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 88.6 hadi utakapo kamilika

No comments:

Post a Comment