WAUMINI wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda waliofunga ndoa kanisani wametakiwa kuvaa pete zao za ndoa muda wote, ili kuendeleza kiapo cha Agano Takatifu la Ndoa, la sivyo hawataruhusiwa kupokea Komunio Takatifu kanisani humo.
Uamuzi huo umetolewa na Paroko Msaidizi wa Kanisa hilo, Padri Cletus Bafumeko, wakati akitoa mahubiri yake katika Ibada ya Jumapili iliyopita.
Huku akishangiliwa kwa vigelegele na waumini waliofurika kanisani humo, Padri Bafumeko alitoa karipio kuwa atahakikisha katika kila ibada, wanandoa wote wasio na pete zao za ndoa vidoleni, wanazuiwa kushiriki Sakramenti Takatifu.
Alisema amelazimika kutoa karipio hilo, kutokana na tabia ya waumini wengi wenye ndoa, kuzoea kuacha pete zao za ndoa wanapokuwa mitaani. Kwa mujibu wa Padri Bafumeko, lengo la waumini hao ni kuonekana mbele za watu kuwa hawana wenzi waliofunga nao ndoa kwa lengo la kujitafutia ‘nyumba ndogo’.
“Sasa tabia hiyo imeendelea kukomaa katika jamii ya waumini wengi wa Kanisa hili na hata wa makanisa mengine, kushindwa kushika kiapo cha Agano Takatifu la Ndoa, kwa kukwepa kuvaa pete za ndoa vidoleni na kusababisha maadili ya ndoa kuporomoka katika jamii.
“Imekuwa sasa kama ni tabia ya waumini wa Kanisa hili, hususani wanandoa, kuvaa pete za ndoa wanapokuwa majumbani, lakini wanapotoka nje ya nyumba, pete huvuliwa na kuwekwa mifukoni au mikobani.
“Nimechunguza sana vidole vyenu ninapokutana nanyi wanandoa mitaani, nikaamua kuangalia hata mnapokuja hapa kanisani, hamvai pete zenu za ndoa kabisa, licha ya kuwa zimebarikiwa kabla ya kukabidhiwa kanisani, ni ishara ya kukosa uaminifu,” alisema Padri Bafumeko.
Alisema katika jamii nyingine, ishara ya kuvunjika ndoa ni kuvua pete na tendo la kuvua pete hiyo huwa ni mwisho wa uhusiano baina ya wanandoa hao.
Hivi karibuni, Kanisa Katoliki limekuwa likibuni mbinu mbalimbali za kurejesha maadili ya waumini wake, ikiwamo ya kuwavisha kaniki wanaokwenda kanisani na vimini, mavazi ya kuacha matiti nje na milegezo.
Parokia kadhaa za Kanisa Katoliki zilitangaza kuandaa mpango wa kuwavisha vazi la kaniki waumini hao ili kukomesha uvaaji mbovu unaokwenda kinyume cha maadili.
Paroko wa Msewe, Dar es Salaam, Padri Piero Clavero na viongozi wa Baraza la Walei katika Parokia hiyo ndio waliotoa tangazo hilo siku chache zilizopita.
Mwenyekiti Msaidizi wa Parokia, Benedict Fungo, alikiri kutolewa kwa tangazo hilo na kudai kuwa halina lengo la kumfukuza mtu kanisani, bali kurejesha nidhamu.
“Ni kweli tulitangaza, lakini hatukulenga kufukuza watu kanisani, lengo ni kurejesha maadili kwa waumini hasa vijana, unajua kanisani ni nyumba ya ibada, mtu anakwenda kupokea Ekaristi, ameacha matiti nje, wamevaa nguo zinaitwa za kupiga jeki, tukumbuke na mapadri ni binadamu jamani,” alisema Fungo.
Fungo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Liturjia ya Parokia yenye dhamana ya kusimamia maadili, alisema baada ya tangazo hilo, yametokea mabadiliko makubwa na hakuna aliyevishwa kaniki hadi sasa.
No comments:
Post a Comment