Monday, March 12, 2012

TBS Wafanya Ufisadi wa Kutisha


Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali Ludovic Utoh
WAKATI kukiwa na taarifa za ukata Serikalini, imebainika kuwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limefanya ufisadi kupitia mpango wa ukaguzi wa magari nje ya nchi kabla ya kuletwa nchini, hivyo kulikosesha taifa  mamilioni ya fedha.
Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali, imethibitisha kwamba hadi kufikia mwishoni mwa waka jana, Serikali ilikuwa imekosa kiasi cha Sh243 milioni kufuatia hatua ya TBS kushindwa kukusanya ada kutoka kwa kampuni zilizopewa leseni za kukagua magari katika nchi mbalimbali duniani.  Taarifa pia imebaini udanganyifu uliodaiwa kufanyika kwenye tozo za faini kwa magari yaliyodaiwa kuingizwa nchini bila kukaguliwa.

Hali kadhalika, Serikali ilipoteza mapato baada ya  TBS kutoa msamaha kwa maduhuli bila kufuata taratibu za fedha.  Taarifa hiyo ambayo gazeti hili limeiona, inakwenda kwa kamati za Bunge za Hesabu za Serikali na ile ya Hesabu za Mashirika ya Umma na huenda ikawasilishwa katika mkutano wa saba wa Bunge la kumi,utakaofanyika Aprili mwaka huu mjini Dodoma.  “Kwa sasa shirika (TBS) linatoza kiasi cha asilimia 25 ya gharama ya ukaguzi kwa kila gari linalokaguliwa na wakala.

Hata hivyo baadhi ya wakala wameshindwa kuwasilisha kiasi hicho kwa wakati na wengine kushindwa kabisa kuwasilisha mapato yaliyokusanywa kwa mujibu wa makataba uliopo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.  Hata hivyo alipotafutwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Joyce Mapunjo, alionyesha kushangazwa na ripoti hiyo, huku akifafanua kuwa uchunguzi wa Mkaguzi Mkuu wa Serikali bado haujaanza.

 “Hiyo fedha kwa ajili ya kufanyia uchunguzi bado haijapatikana sasa hiyo ripoti wewe umeipata wapi,” alihoji na kuongeza, “hakuna kitu kama hicho.”

Kwa jumla taarifa hiyo inabainisha udhaifu mkubwa katika utendaji kiasi cha kutoa mapendekezo yanayoitaka Serikali kupitia Bodi ya Wakurugenzi wa TBS, kuwawajibisha watendaji wakuu wa shirika hilo akiwamo Mkurugenzi Mkuu, Charles Ekelege.  
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serilali pia alibaini kuingizwa nchini kwa kiwango kikubwa cha bidhaa zinazohatarisha afya za watumiaji kwa kuwa chini ya kiwango au kukosekana wa  taarifa za ziada kuhusu bidhaa ambazo zilibainika kutofaa kwa matumizi ya watu baada ya kufikishwa nchini.
Soma zaidi :http://www.mwananchi.co.tz/biashara/13-biashara-za-kitaifa/20951

No comments:

Post a Comment