BAADHI ya walimu wanaofanya kazi katika Mkoa mpya wa Njombe, wamesema hawana imani na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa madai kuwa ni mawakala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Walimu hao walitoa madai hayo juzi baada ya kikao cha maofisa elimu kilichoketi katika ukumbi wa shule ya Msingi Mwembe Togwa iliyopo eneo la Makambako mkoani humo.
Walisema CWT imekuwa mstari wa mbele kuwakatisha walimu kudai haki zao huku mfumo wa kujiunga na chama hicho ukiwa wa lazima kwa kila mwalimu bila ushirikishwaji.
Mwalimu Fredy Mhanze alisema licha ya yeye kuwa katika taaluma hiyo kwa miaka 15 alilazimishwa kujiunga na chama hicho na tangu wakati huo hajawahi kushirikishwa kwa namna yoyote.
“Tunaingizwa kwenye chama kwa lazima huku hakuna ushirikishwaji, tunaktwa fedha zetu kuwachangia wachache huku tukikatwa kodi. Mimi nakatwa sh 12,000 kila mwezi,” alisema na kuongeza ameamua kuungana na walimu wenzake kuanzisha na kusajili chama chao cha hiari.
kwa upande wake, Mwalimu Siyomena Ndunguru alisema serikali kwa kushirikiana na CWT imeshindwa kufuta waraka kandamizi kwa walimu ambao unamfanya mwalimu kuwa mtumwa na kumnyima haki ya kujiendeleza kielimu.
Akifafanua alisema madai ya waraka huo kandamizi ni pamoja na kuwa mwalimu yeyote anayetaka kujiendeleza lazima ajilipie mwenyewe wakati taratibu za utumishi ni mtumishi anatakiwa kulipiwa karo.
pamoja na hayo, alisema kwa sasa mwalimu wa kike anapotaka uhamisho kwa ajili ya kumfuata mumewe sehemu anayofanyia kazi, halipwi jambo ambalo inaonekana dhahiri unyanyasaji wa kijinsia huku CWT ikiendelea kulifumbia macho suala hilo.www.freemedia.co.tz
No comments:
Post a Comment