Thursday, March 15, 2012

Mihuri Yadaiwa Kutumika Kuchakachua Matokeo Ya Chaguzi!

ALIYEKUWA Meneja kampeni wa Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Abdulrahaman Kinana, amehusishwa na uchakachuaji wa matokeo ya Ubunge katika Jimbo la Segerea mkaoni Dar es Salaam.
Kinana alidaiwa kuhusika katika uchakachuaji wa matokeo hayo na shahidi wa sita katika kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo, Livingstone Rugema wakati akitoa ushahidi wake mahakamani jana.

Shahidi huyo alitoa madai hayo kwa nyakati tofauti wakati akitoa ushahidi wake, akiongozwa na wakili wa Mpendazoe, Peter Kibatala na wakati akihojiwa na mawakili wa utetezi, Jerome Msemwa na Wakili wa Serikali (SA) David Kakwaya.

Wakati Kinana akidaiwa kuhusika katika uchakachuaji wa matokeo hayo, Mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk Makongoro Mahanga jana aligongana uso kwa uso mahakamani hapo na mpinzani wake Fredy Mpendazoe.

Dk. Makongoro aliibuka mahakamani hapo jana ghafla ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kesi hiyo ianze kusikilizwa ambapo alisalimiama na Mpendazoe, kisha baadaye wakati akiondoka, akamuomba Mpendazoe afute kesi hiyo ili mwaka 2005 amwachie jimbo hilo.

Kesi namba 98 ya mwaka 2011 inayosikilizwa na Jaji Profesa Ibrahim Juma, ilifunguliwa na Mpendazoe aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akipinga ushindi wa Dk Mahanga.

Wakati Wakili Kibatala akimwakilisha Mpendazoe katika kesi hiyo, Wakili Msemwa anamtetea Dk Mahanga, huku SA Kakwaya akiwatetea Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo ya manispaa hiyo.

Wakati akitoa ushahidi wake na wakati akihojiwa na mawakili hao wa utetezi, shahidi huyo kwanza alidai kuwa yeye alikuwa wakala wa majumuisho wa Chadema katika Kata ya Segerea na kwamba baadaye alikwenda Anatoglou mahali ambako matokeo ya jimbo hilo yalikuwa yakijumlishwa na kutangazwa.

Alidai kuwa wakati wakisubiri matokeo kutangazwa Novemba 2 mwaka 2010 majira ya jioni, Kinana alifika kituoni hapo kisha akaondoka na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo ya Ilala.

Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa matukio yaliyojitokeza baadaye baada ya Kinana kuondoka kituoni hapo Anatoglou, yalitia mashaka kiasi cha kumhusisha Kinana na Mkurugenzi huyo kuwa walikwenda ‘kupika matokeo.’

Shahidi Rugema aliyataja matukio hayo kuwa ni pamoja na kijana mmoja kukamatwa na mihuri, mtendaji wa Kata ya Tabata, Imelda Kafanabo kukamatwa na fomu za matokeo pamoja na Mtendaji wa Kipawa pia kufika Anatoglou akiwa na fomu peke yake bila mawakala wala polisi.

Alipoulizwa na SA Kakwaya kama wakati wakitoka Kinana na Mkurugenzi aliwaona wamebeba kitu chochote ,shahidi Rugema alijibu kuwa hakuona kitu chochote wala wakati wakiingia hakuwaona.

Lakini alidai kuwa Mkurugenzi aliyeaminiwa kusimamia uchaguzi huru na wa haki, kuonekana akiongozana na mmoja wa wanachama wa vyama vinavyopingana bila kuwepo kwa mawakala wa vyama vingine wala polisi na kwenda mahali kusikojulikana, kilitia shaka.

Alisisitiza kuwa matukio yasiyo ya kawaida yaliyotokea baadaye ikiwamo kukamatwa kwa mihuri na fomu za matokeo na kuonekana kwa watu wasiohusika, inaonesha kuna mahali matokeo hayo yalikwenda kupikwa na kwamba matokeo hayo yaliyotangazwa hayakuwa halali.

“Hata kama alikuwa mmoja wa mawakala wa kura za urais katika jimbo mojawapo (Kinana), lakini kuondoka wenyewe bila mawakala wengine walikwenda kufanya nini? Angetuambia kule walienda kufanya nini na angeongozana na watu wengine,” alisisitiza shahidi Rugema.

Akijibu swali la SA Kakwaya jinsi mihuri hiyo ilivyoweza kuathiri matokeo ya Segerea, shahidi Rugema alidai kuwa kitendo cha mihuri hiyo kuonekana eneo la kujumlishia matokeo na siyo kituo cha kupigia kura, kilifanya uchaguzi huo uonekane si huru na wa haki.

“Hivyo ninaona kuwa matokeo hayo yalipikwa tu. Kulingana na matokeo yaliyokuwa yamebandikwa ukutani Mpendazoe kuna sehemu nyingi alikuwa akiongoza lakini baadaye ikatangazwa kwamba Makongoro ameshinda, naona kuwa mihuri hiyo ndio ilitumika kupika matokeo hayo.

Alidai kuwa katika Kata ya Segerea alikosimamia yeye, majumuisho Mpendazoe alishinda kwa kura 5,496 huku Dk Mahanga akipata kura 3,954.

Shahidi huyo alidai kuwa hata taratibu za utangazaji wa matokeo zilikiukwa kwani matokeo ya kila kituo hayakutangazwa na kwamba hata msimamizi wakati akitangaza matokeo hayo, hakuwa katika hali nzuri huku akiwa chini ya ulinzi mkali.

“Mkurugenzi alipotangaza matokeo hakuwa katika ‘mood’(hali) nzuri kama tuliyozoea kumuona ofisini. Alitakiwa kuonekana mwenye furaha kwenda kumtangaza mshindi kwa zoezi alilosimamia yeye, lakini hakuwa hivyo,” alisisitiza shahidi huyo.

Kwa upande wake Shahidi wa saba, Mwangalizi wa Dawati la Uchaguzi kutoka Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC), Merick Luvinga alidai kuwa waliweka waangalizi wa uchaguzi nchini kote na kila kituo katika majimbo 24 yalioonekana kuwa na upinzani.

Alidai kuwa Segerea zilitokea dosari mbalimbali na kwamba waliandika ripoti kwenda Tume ya Uchaguzi iliyosimimamiwa na Profesa Peter Maina, wakipendekeza namna ya kuboresha chaguzi zijazo.

Hivyo aliiomba mahakama imwamini akidai kuwa ana uzoefu wa uangalizi wa chaguzi mbalimbali ndani na nje na kwamba katika ripoti zao, hawajawahi kulalamimikiwa kuwa wamependelea upande mmoja.

Kabla ya kesi hiyo kuanza asubuhi Dk Mahanga alifika mahakamani hapo na kumkuta Mpendazoe ambapo walisalimiana na kisha wakaendelea kusikiliza kesi wakati shahidi wa sita akitoa ushahidi.

Baadaye wakati akitoka nje ili aondoke Dk Mahanga alimkuta Mpendazoe nje ndipo akamwambia katika hali ya utani kuwa aifuete kesi hiyo, ili yeye amalizie muda uliobaki halafu atamwachia jimbo hilo mwaka 2015, lakini Mpendazoe hakumjibu chochote.

Katika kesi hiyo Mpendazoe analalamikia mwenendo mzima wa uchaguzi katika jimbo hilo akida taratibu na sheria za uchaguzi zilikiukwa katika ukusanyaji ujumulishaji na utaratibu wa kuhesabu na utangazaji wa matokeo.

Hivyo anaiomba Mahakama hiyo itengue matokeo ya ushindi wa mbunge aliyetangazwa na kuamuru ufanyike uchaguzi mdogo, au yeye atangazwea mshindi.Chanzo: Gazeti Mwananchi jana Jumatano.

No comments:

Post a Comment