Friday, March 2, 2012

Siyoi Ambwaga Tena Sarakikya




Waandishi Wetu, Arusha
KWA mara ya pili, wana CCM Jimbo la Arumeru Mashariki wamedhihirisha kuwa chaguo lao ni Siyoi Sumari baada ya kumchagua kwa kura 761 na kumtupa mbali mpinzani wake, William Sarakikya aliyepata kura 361 katika uchaguzi wa marudio uliofanyika jana.Matokeo hayo ni kama ushindi kwa mojawapo ya kambi ndani ya CCM inayohusishwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa dhidi ya wanachama waliopo katika makundi mengine, ambayo yalikuwa yakipinga kwa nguvu zote kupitishwa kwa jina la Siyoi.

Vyombo mbalimbali vya habari kwa wiki nzima sasa, vimekuwa vikiripoti kuhusu mgawanyiko ndani ya chama hicho tawala kutokana kuwa na misimamo inayokinza kuhusu nani atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo mdogo.

Siyoi alianza kuzua mtafaruku ndani ya CCM pale suala la uraia wake lilipozua utata ndani ya kikao cha Sekretarieti ya chama hicho, hivyo kusababisha kutolewa kwa mapendekezo kwamba aenguliwe katika kinyang’anyiro hicho.

Kundi linalomtetea limekuwa likilalamikia kile linachodai kwamba ni kuwapo kwa njama za kumtosa mshindi huyo kwa sababu kadhaa za kimakundi.

Hata hivyo, Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichokutana chini ya Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete kiliamuru kurudiwa kwa uchaguzi baina ya Siyoi na Sarakikya, kwa maelezo kwamba katika wagombea wote sita hakuna aliyekuwa amepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.

Habari zaidi zilidai kuwa, hata baada ya kutolewa kwa uamuzi wa kurudiwa kwa uchaguzi huo, mmoja wa vigogo wa CCM alituma mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu kwenda kumshawishi Siyoi ajitoe kwenye kinyang’anyiro hicho, jitihada ambazo hazikufanikiwa kwani alikataa.

Matokeo ya kura
Matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa Saa 11:30 jioni na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, Sumari aliibuka na ushindi huo wa silimia 67.8 kati ya kura halali 1,122 zilizopigwa, dhidi ya asilimia 32.2 za mpinzani wake anayedaiwa kupigiwa chapuo na viongozi wa chama na Serikali kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi taifa.

Jumla ya kura 1,124 zilipigwa ambapo mbili ziliharibika na kura halali kubakia 1,122.

Akitangaza matokeo hayo, Msekwa alilazimika kuanza kwa kumtangaza mshindi hali iliyofanya ukumbi kukosa usikivu kwa wapenzi, mashabiki na wafuasi wa Siyoi kuanza kushangilia.

Msekwa alisema ameridhishwa na upigaji kura na matokeo hayo yameonyesha imani kubwa waliyonayo wana Arumeru kwa mgombea huyo.

Baadhi ya wana CCM walidai kuwa kauli tata za Msekwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Chiligati katika ufunguzi wa mkutano mkuu maalum wa Wilaya ya Arumeru jana zilimponza, Sarakikya baada ya wajumbe kuamua kupiga kura za hasira wakipinga kile walichodai kushinikizwa kumchagua mtu aliyeelezwa anatakiwa na mfumo (system), wa Serikali na uongozi wa chama.

Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliohudhuriwa na idadi kubwa ya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), maofisa usalama wa taifa na askari kanzu kutoka Jeshi la Polisi, Msekwa na Chiligati waliwataka wajumbe kutumia vyema kura yao kumchagua mtu atakayemudu na kuhimili vishindo vya upinzani kutoka vyama vingine vitakavyosimamisha wagombea.

“Ndugu wajumbe napenda kuwakumbusha jambo moja muhimu kabla ya kupiga kura, leo hatuchagui mbunge, mnachofanya ni kupiga kura za maoni. Mgombea atateuliwa na kikao cha Kamati Kuu Machi 3, mwaka huu,” alisema Chiligati.

Wakati Chiligati akisititiza hoja hiyo, Msekwa alikuwa akitikisa kichwa kuonyesha kukubaliana na maneno aliyokuwa akiyasema Naibu Katibu Mkuu huyo huku baadhi ya wajumbe wakiguna.

Msekwa aliyetumia muda mwingi kuzungumzia historia yake ya uongozi ndani ya chama kuanzia TANU hadi CCM aliwataka wajumbe kutoangalia uswahiba wala ushawishi wa aina yoyote katika maamuzi yao bali wahakikishe wanayemchagua anastahili kupeperusha bendera ya chama hicho tawala na kukiletea ushindi.

Siyoi Sumari akiwa amebebwa na wafuasi wa CCM baada ya kuibuka mshindi wa kura za maoni za mgombea Ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia chama hicho, jana. Picha na Filbert Rweyemamu

Katika uchaguzi wa awali wa kura za maoni uliofanyika Februari 20, mwaka huu, Siyoi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremia Sumari aliyefariki hivi karibuni aliongoza kwa kupata kura 361 akifuatiwa na Sarakikya alijinyakulia kura 259.

Wagombea wengine na kura walizopata katika uchaguzi wa awali kwenye mabano ni pamoja na Elirehema Kaaya (205), Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Elishilia Kaaya (176), Antony Msami (22) na Elishiankira Urio aliyeambulia kura 11.

Msami tayari amehamia Chadema alikochukua fomu kuomba uteuzi wa kupeperusha bendera ya chama hicho na kuambulia kura 8 katika uchaguzi wa kura za maoni ndani ya chama hicho zilizopigwa juzi eneo la Maji ya Chai wilayani Arumeru.

Kamatakamata ya Takukuru
Katika hatua nyingine, kitendo cha kuwakamata baadhi ya viongozi na makada wa chama hicho juzi kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa lengo la kumsaidia mmoja wa wagombea jana kilibadilisha upepo miongoni mwa wapiga kura ambao wengi walidai kitendo hicho kililenga kumnufaisha mmoja wa wagombea na hivyo kuazimia kuonyesha hasira yao kwenye sanduku la kura.

Miongoni mwa viongozi na makada wa CCM aliyekamatwa kwa kudaiwa kujihusisha isivyo halali katika kampeni za Siyoi ni pamoja na Diwani wa Kata ya Mbuguni, Thomas Mollel maarufu kwa jina la ‘Askofu’ aliyesema baada ya kutiwa mbaroni kwa maagizo ya watu aliowaita wakubwa, alihojiwa kwanini anamfanyia kampeni mgombea huyo na aliyemtuma kufanya hivyo.

Ingawa kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Mbengwa Kasomambuto alikataa kuwataja viongozi wengine walioshikiliwa juzi kwa mahojiano, waandishi wetu waliofika ofisi za taasisi hiyo walimshuhudia mmoja wa waliogombea katika awamu ya kwanza ya kura za maoni pamoja katibu wa UVCCM katika moja za Wilaya za Mkoa wa Arusha wakihojiwa na maafisa wa idara hiyo ya dola.

Katika orodha hiyo pia walikuwapo madiwani wawili wa Kata za Arumeru na jana eneo lote la mkutano ulijaa maafisa wa Takukuru, na askari kanzu waliokuwa wakiranda kila kona na kujisogeza kwenye kila kundi la watu zaidi ya wawili walioonekana kuzungumza kwa lengo la kunasa mazungumzo yao...Soma zaidi www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment