Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya madaktari kutishia kuanza mgomo
mwingine, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema amesikitishwa na tishio hilo
akisema kwa sasa Serikali ipo katika mchakato wa utekelezaji wa makubaliano
mbalimbali na wanataaluma hao.
Pinda alitoa kauli hiyo jana aliokuwa akizungumzana
katika mahojiano maalumu na Gazeti dada la Mwananchi, The Citizen na kusema
hatua hiyo mpya ya madaktari inamsikitisha kwa kuwa Serikali ndiyo kwanza
inaendelea na vikao kwa ajili ya kuangalia namna ya kutekeleza madai yao
hayo.
“Siwezi kuzungumza chochote sasa wakati Serikali
inaendelea kushughulikia mgogoro huo. Niseme tu kwa kweli wananisikitisha
(madaktari). Ninasikitika kuona kwamba wakati bado tuko kwenye mazungumzo,
wenzetu wanafanya vikao vingine,” alisema Pinda.
Akilihutubia taifa Februari 29 mwaka huu, Rais Jakaya
Kikwete alieleza kufurahishwa na hatua ambayo suala hilo limefikia
akisema:“Nashukuru mgomo huo umekwisha lakini makovu yake yatabaki maisha katika
kumbukumbu za historia ya taaluma ya tiba hapa nchini.”
“Leo (Februari 29), Mheshimiwa Waziri Mkuu amenipa
taarifa kuwa kamati aliyounda kushughulikia madai ya madaktari imekamilisha kazi
yake na kuwasilisha taarifa yake kwake. Kuanzia kesho (Machi, Mosi), Serikali
itaifanyia kazi taarifa hiyo na kuamua ipasavyo kulingana na uwezo uliopo.
Ninawaomba ndugu zetu madaktari kuwa na moyo wa subira.”
Rais Kikwete alisema Serikali inatambua, inajali na
kuthamini kazi za madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya katika kulinda
na kudumisha afya za Watanzania hivyo itajitahidi kuona kuwa inafanya kila
liwezekanalo kuhakikisha kuwa mgomo haujirudii tena.
Hata hivyo, wakati Pinda akieleza kusikitishwa na hatua
hiyo mpya ya madaktari, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya
alisema hawezi kujiuzulu kama madaktari hao wanavyotaka kwa kuwa suala hilo liko
nje ya uwezo wake.“Hivi sasa siwezi kuzungumza chochote kwa kuwa suala hilo liko
juu yangu na siwezi kujiuzulu,” alisema Dk Nkya.
Tishio la madaktari
Juzi, madaktari hao waliipa Serikali siku tatu kuanzia
jana hadi Jumatano wiki hii kuhakikisha inawatimua kazi Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Hadji Mponda na Naibu wake, Dk Nkya vinginevyo watatangaza mgomo
mwingine waliouita wa kihistoria.
Pia, madaktari hao kupitia kwa wawakilishi wao waliopo
katika kamati iliyoundwa na Pinda kujadili madai yao, wamekubaliana kutoendelea
na majadiliano hadi hapo mawaziri hao watakapoondolewa kwenye nyadhifa
zao.
Hatua hiyo imekuja zikiwa zimepita siku chache baada ya
kikao kilichoitishwa na Serikali kujadili suala hilo kuvunjika huku kila upande
ukituhumu mwingine kuhusika.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa
madaktari hao ulifanyika Dar es Salaam juzi, Rais wa Chama cha Madaktari
Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi alisema kama mawaziri hao wataendelea na
nyadhifa zao hadi Jumatano, madaktari hawatakuwa tayari kuendelea na
kazi.
“Madaktari wameona isingekuwa jambo jema kuendelea
kujadiliana na kufikia uamuzi na Serikali huku Waziri na Naibu wake wakiendelea
kushikilia nyadhifa zao, watu hao wanawajibika kwa kila kilichotokea? Nani
asiyejua kuwa vifo vilitokea wakati wa mgomo?” alisema Dk Mkopi na
kuongeza:
..Soma zaidi www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment