(Pichani kulia.)
NIMEKUWAPO Arumeru Mashariki kwa zaidi ya wiki mbili sasa, nikifuatilia kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge ambao umepangwa kufanyika Jumapili ijayo, Aprili 1, 2012.
Kwa ujumla kampeni hizi zimekuwa za kistaarabu zaidi ikilinganishwa na zile za mwishoni mwa mwaka jana wilayani Igunga ambako pia kulifanyika uchaguzi mdogo na CCM kuibuka washindi kupitia kwa mgombea wake, Dk Dalaly Kafumu.
Waandishi wa habari tunaoandika matukio ya kampeni hizi ndiyo tunaotizamwa na Watanzania wote kuwapa kile kinachotokea kwani si wote wanaoweza kufika Arumeru Mashariki, lakini kinyume chake tunatia aibu kiasi cha kutisha.
Vyombo vya habari vinawajibika kwa umma wa Watanzania walio wasomaji wa magazeti yetu, wasikilizaji wa radio zetu na hata watazamaji wa luninga zetu.
Jambo moja ni dhahiri kwamba katika hadhira hii ambayo ni wateja wetu wapo wenye itikadi mbalimbali, ziwe za kisiasa, kidini na nyinginezo lakini pia wapo wasiokuwa na itikadi zozote zile, wao ni Watanzania, wala hawafungamani na upade wowote. Wote hawa tunapaswa kuwatumikia.
Nijuavyo mimi sisi tunaoripoti habari za uchaguzi haimaanishi kwamba bora zaidi kuliko waandishi wa habari wengine la hasha, bali tumeaminiwa kutenda kwa niaba ya wenzetu wengi ambao pia wana uwezo kama wetu.
Kwa kifupi naweza kusema tuko zamu na pengine kukiwa na uchaguzi mwingine tunaweza kupewa zamu nyingine, au wakapewa wenzetu.
Ni kwa bahati mbaya kwamba sisi tulioaminiwa kufanya kazi ya kuripoti habari za kampeni za Arumeru Mashariki tumejisahau, kiasi cha kufanya kazi ambazo si zetu. Tumeacha maadili namisingi ya kazi zetu, tumeingia katika ushabiki wa vyama jambo ambalo si hatari tu kwa mustakabali wa demokrasia ya nchi yetu bali hata kwa maisha ya taaluma ya habari nchini.
Waandishi wa habari katika kampeni hizi matendo yetu yanawatia kuchefuchefu hata makada wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi, kwani tumechukua kazi zao na tumegeuka kuwa makada na wakereketwa wa siasa kuliko wao. Hii si kazi yetu.
Uswahiba huu na vyama vya siasa umetufanya kushindwa hata kuandika ukweli wa kile kinachotokea kwenye mikutano ya kampeni. Tunafikia mahali pa kuweka makubaliano ya kijinga ya kuua habari kwasababu tu ya ukereketwa wetu, sijui hili kwa maslahi ya nani!.
Tumejengea baadhi ya waandishi wenzetu uhasama wa hali ya juu kwa kuwa watoa taarifa kwa viongozi wa kisaisa, tukibaguana kwamba huyu ni wa chama fulani, si mwenzetu na yule ni mwenzetu si kwa misingi ya taaluma ya habari bali kwa misingi ya vyama tunavyoviandikia habari.
Badala ya kuwaandikia Watanzania, wenye uchu na shauku ya kufahamu mchakato wa demokrasia unavyokwenda Arumeru Mashariki, basi tunaviandikia vyama vya siasa vinavyoshiriki, hili si sawa kabisa na halikubaliki.
Hali hii imetufikisha pabaya kwani katika kampeni hizi wapo waandishi wa habari hawawezi kufika katika kambi za vyama vingine kwani wao wamejibagua tayari kwamba wanautumikia mlengo wa kushoto au mlengo wa kulia.
Nasema hivi kwa mifano hai kwani wengine ‘tumeshtakiwa’ na waandishi wenzetu kwa wanasiasa hawa, kwamba eti tupo kwa ajili ya kuhujumu vyama fulani, lakini kwa hulka ya wanasiasa walivyo mwishoni mwa siku wanatufikishia taarifa hizi, na kuwataja wale waliopeleka ‘mashtaka’.
Katika haya tumeruhusu hata wanasiasa kutupangia aina ya habari tunazopaswa kuziandika na kuzituma kwenye vyombo vyatu vya habari, hii ni aibu na fedheha kubwa kwa taaluma yetu na waandishi ambao tuna tabia za aina hii.
Hatuwezi kuacha tabia za aina hii kuendelea, lazima tuchukue hatua kama wanataaluma kwani kuziacha ni sawa na kuiweka taaluma ya habari rehani.
Kama walivyo Watanzania wengine, waandishi wa habari nchini tuna uhuru wa kuwa wananchama wa vyama vya siasa, kushiriki uchaguzi na kuwachagua viongozi katika chaguzi mbalimbali.
Lakini lazima tujitambue kwamba, kitaaluma tunapaswa kuwa juu ya ushabiki wa siasa za vyama, kwani kwa kufanya hivyo tu ndipo tunaweza kutekeleza wajibu wetu kwa Watanzania kwa haki.
Tunapofanya kazi kwa ushabiki na upenzi wa kupitiliza tujue kwamba hatuwatendei haki walaji wa habari zetu ambao kwao habari ni zaidi ya vyama, siasa na wanasiasa.
Wakati wadau na wanataaluma wa habari tukiendelea kutafakari jinsi ya kuikwamua taaluma hii hasa tunapokwama kwenye mitego ya kisiasa iwe kwa kupenda sisi wenyewe au kwa sababu nyinginenezo, ni wajibu wa kila mwandishi wa habari ajitambue kwamba ana wajibu upi kwa umma.
Vinginevyo basi anayedhani kwamba taaluma hii inambana asitekeleze mapenzi yake ya kisiasa iwe ni kwa chama ama kwingineko, ajiengue mapema kwani kuondoka si dhambi, wapo wengi wamefanya hivyo na maisha yanaendelea.
No comments:
Post a Comment