Monday, March 26, 2012

Akina Mama Wajawazito 1600 Wanafariki Kila Mwaka...


 Na watoto elfu 27 hufariki dunia.
Na Mwandishi wetu
ZAIDI ya watoto elfu 27, na akinamama wajawazito 1,600, wanafariki

kila mwaka kutokana na tatizo la upungufu wa viini lishe na madini ya
chuma mwilini.

Akizungumzia tatizo hilo Dr. Celestin Mgoba ofisa lishe mwandamizi,
kutoka taasisi ya chakula na lishe amesema tatizo hilo linalopunguza
tija kwa Taifa katika uzalishaji, kwa zaidi ya asilimia 17.

Dr. Mgoba amesema kwa kutambua uwepo wa tatizo hilo wizara imeanzisha
mpango wa kuongeza viini lishe katika chakula, kwa kuwa watoto zaidi
ya asilimia 36 mkoani Iringa wana upungufu wa Vitamini “A”.

Naye Dr. Subilaga Kazimoto kutoka wizara ya jamii na ustawi wa jamii,
idara ya kinga kitengo cha lishe amesema Iringa ni kati ya mikoa
mitatu yenye tatizo la Utapiamlo, na kuwa watoto wenye umri wa miezi 6
hadi miezi 24 wanasumbuliwa na ugonjwa huo.

Dr. Kazimoto amesema wizara imeanzisha mpango wa kuboresha lishe kwa
kuongeza viini lishe ili kuongeza nguvu kazi kwa Taifa ambayo imepotea
kwa asilimia 17 na kudumaza uchumi.

Naye bwana afya mkoa wa Iringa, Dr. Rika Ngaga amesema mkoa
unakabiliwa na tatizo la Utapiamlo mkali kutokana na jamii kutokuwa na
mpangilio mzuri wa vyakula, licha ya kuzalisha chakula kwa wingi.

No comments:

Post a Comment