Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Sensa, Dk. Albina Chuwa akisisitiza jambo.
Na. Mwandishiwetu - MAELEZO
Morogoro.
Ikiwa imebaki miezi michache kabla ya kuanza kwa zoezi la Sensa ya watu na makazi nchini serikali imewataka waratibu wa zoezi hilo kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu fedha na rasilimali zinazopelekwa kwenye mikoa na wilaya zote nchini ili kufanikisha zoezi hilo.
Akizungumza na waratibu wa Sensa ya watu na makazi 2012 kutoka katika mikoa na wilaya zote nchini leo mjini Morogoro naibu katibu mkuu Ofisi ya Waziri mkuu ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw.Alphayo Kidata amesema kuwa zoezi hilo litafanikiwa kwa kiwango kikubwa kama waratibu hao watasimamia ipasavyo matumizi ya fedha na rasilimali zinazopelekwa katika meneo yao.
Amesema jukumu la usimamizi wa Sensa kwenye ngazi ya mikoa na wilaya ni la viongozi wa maeneo hayo na kufafanua kuwa kushindwa kwa zozei hilo katika wilaya au mikoa husika ni kiashirio cha viongozi hao kushindwa kusimamia majukumu yao kwani takwimu zitakazopatikana zitatumiwa pia na mamlaka za mikoa na wilaya katika shughuli za maendeleo.
"Napenda kusisitiza kuwa mafanikio ya Sensa ya watu na makazi 2012 yanawahusisha pia viongozi wa mikoa na wilaya zote nchini hivyo usimamizi usioridhisha kwenye mikoa na wilaya zetu utasababisha upatikanaji wa takwimu zisizosahihi na hivyo kuathiri maendeleo ya maeneo hayo hivyo tunawajibu wa kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa" amesisitiza.
No comments:
Post a Comment