Tuesday, June 12, 2012

Maafisa Habari Wa Serikali Waaswa

Mh.waziri,Dkt.Fenela Mukangara

Na Magreth Kinabo ( Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo)
 
IDARA ya Habari ( MAELEZO) imetakiwa kujipanga vizuri ili kuweza kutekeleza majukumu yake ya kuwa Msemaji wa Serikali ipasavyo; hatua hiyo itasaidia kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na utendaji wa Serikali.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali katika ukumbi wa Victoria Palace Jijini Mwanza.
Aidha, Dkt. Mukangara alisema, Idara ya Habari ( MAELEZO) ina jukumu zito la kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali . Hii ni kwa mujibu wa agizo la Serikali Na. C 16 la mwaka 1977.
" Serikali inafanya mambo mengi mazuri kwa wananchi lakini hayasemwi. Matokeo yake Serikali inaishia kulaumiwa na wananchi bila sababu.
"Ndugu zangu hali hii haikubaliki. Lazima tubadilike na lazima tuseme . Hatuwezi kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali asiyesema." Alisema Dkt. Mukangara.
Dkt. Mukangara aliongeza kuwa Idara ya habari itekeleze jukumu hilo kwa kushirikiana na Wasemaji wa Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali na Wasemaji hao watambue kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ni Idara ya Habari.
Akizungumzia kuhusu uhuru wa vyombo vya habari alisema,tunalo tatizo la baadhi ya vyombo vya habari nchini kudhani kwamba uhuru wa vyombo vya habari hauna mipaka. Hivyo alivitaka vyombo vya habari vitambue kuwa hakuna nchi yoyote duniani ambayo utendaji wa vyombo vyake vya habri haubna mipaka.
" Wakati wote uhuru wa vyombo vya habari popote pale huendana na wajibu hata ktika mataifa yaliyoendelea"Alisema Dkt. Mukangara.
Aidha, alivitaka vyombo vya habari kuwa makini katika kutangaza habari zinazohusu mchakato wa mabadiliko ya katiba huku akisissitiza kuonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kuwahabarisha wananchi na kutoa elimu.

No comments:

Post a Comment