Tuesday, April 17, 2012

Rushwa njenje ubunge wa Afrika Mashariki

Mbunge wa Kitope ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd (kushoto) na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge wakielekea katika Ukumbi wa Bunge kuudhuria kikao cha tano cha mkutano wa saba wa Bunge, mjini Dodoma jana.

KAMPENI za lala salama za kuwania nafasi za Ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) mjini hapa, zinadaiwa kugubikwa na rushwa kwa baadhi ya wabunge wakidaiwa kupewa kati ya Sh100,000 na Sh milioni moja.Habari zilizopatikana jana mjini hapa zinaeleza kwamba mbunge mmoja amekabidhiwa kitita cha Sh5 milioni ili kuzigawa kwa baadhi ya wabunge.

Baadhi ya wabunge na wagombea waliohojiwa jana, walithibitisha kuwapo kwa vitendo hivyo vya rushwa huku wakishangaa ukimya wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Naibu Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe alisema ingawa hajafuatwa na mgombea au wakala yeyote akitaka kumhonga, vitendo hivyo ni dhahiri na havina kificho.

“Mgombea anayetoa rushwa ili achaguliwe kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki hatufai kwa sababu anaweza kuuza nchi… tuwakatae wagombea wote wa aina hii ili iwe fundisho,” alisema Zitto.

Alisema mgombea yeyote anayetoa rushwa ili kupata nafasi yoyote ile, iwe ya kisiasa au kikazi, anapoteza sifa ya kuwa kiongozi na kusisitiza kuwa wanaotoa rushwa hawawezi kuwa na uzalendo na nchi badala yake watatanguliza maslahi yao.

Mbunge mmoja wa Kanda ya Ziwa ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema suala la kampeni hizo kutawaliwa na rushwa halina ubishi.

“Mimi mwenyewe juzi alikuja mmoja wa wagombea akataka kunipa Sh300,000 nikamwuliza za nini? Akasema ananipa ni za gharama za simu nimsaidie kampeni. Lakini kesho yake akawa amenisahau akataka kunipa tena Sh200,000,” alidai.

Viwango vya rushwa vinatajwa kutofautiana kulingana na mwonekano na ushawishi alionao mbunge anayelengwa lakini vinavyotajwa ni kati ya Sh100,000 na Sh700,000

"Wabunge wengine wanapewa pia Sh200,000, wengine Sh300,000, Sh500,000 na wapo wengine wanaopewa hadi kati ya Sh700,000 na Sh milioni moja.

Wagombea wanne na ndiyo wanaotajwa zaidi kumwaga fedha hizo za rushwa. Huku ikielezwa kwamba vitendo hivyo vinafanyika kwenye hoteli walizofikia wabunge hao ambazo zimetawaliwa na pilikapilika nyingi.

Mgombea Ubunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere (kulia) akimwinamia Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli wakati akimwomba ampigie kura iliaweze kuchukuwa nafasi hiyo kwa wagombea kutoka Tanzania Bara, Bungeni mjini Dodoma jana.
Mmoja wa wagombea Dk Edmund Mndolwa alisema taarifa za kuwapo kwa rushwa zinazotolewa kwa baadhi ya wabunge naye amezilisikia na kusema Takukuru ijue kuwa panapofuka moshi siku zote chini kuna moto.

“Mimi nimeyasikia hayo kwa mbali kuwa kuna rushwa inatembea na nilipowalalamikia marafiki zangu, wakaniambia niache hofu. Takukuru inapaswa ichunguze hayo na kama yapo ichukue hatua,” alisema Dk Mndolwa.

Mbunge wa Vunjo ambayeb pia ni Mwenyekiti TLP, Augustino Mrema alisema taarifa za kuwapo kwa vitendo vya rushwa imemfikia lakini hajapelekewa fedha hizo kwa vile wanajua angewaumbua.

“Mimi nasikia tu ooh! kuna wa Sh100,000, sijui 300,000 na wengine mpaka milioni lakini mimi hazijanipitia hizo fedha… hakuna mtu amefika kwangu akasema Mrema chukua hizi,” alisema na kuitaka Takukuru ichunguze madai hayo.

Mrema alisema anafahamu ni vigumu kupata ushahidi wa vitendo hivyo kwa kuwa vinafanyika baina ya mtu au watu wanaokubaliana katika jambo moja lakini Takukuru ingeweza tu hata kufanya uchunguzi na kupata ushahidi wa mazingira.

Takukuru yatangaza vita
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmari alipoulizwa jana kuhusu madai hayo alikiri kuwa na taarifa za baadhi ya wagombea na mawakala wao kutoa rushwa na kusema taasisi hiyo imesambaza vijana wake katika kila kona ya mji huo.
Alisema tangu juzi usiku, wamekuwa wakizunguka usiku na mchana kwenye mahoteli na vijiwe vinavyoaminika kutumiwa na wagombea na wapambe wao lakini hawajafanikiwa kuwakamata.
“Taarifa tunazo tangu jana (juzi), hatujalala mimi na vijana wangu tumekesha kuzunguka kila kona lakini tatizo tunalokumbana nalo ni kwamba wale wanaopokea fedha hizo hawataki kutoa ushirikiano,” alisema.
Aliwataka wabunge na watanzania wenye uzalendo na nchi yao kuipatia taasisi hiyo taarifa za siri za watu wanaotoa fedha hizo na wale wanaozisambaza akiwahakikishiwa kwamba majina yao yatalindwa.
“Nawaomba wabunge watusaidie katika hili kwa sababu wao ndiyo walengwa kwa kuwa ndiyo wanaopiga kura. Kama ni kufuatwa wao ndiyo wanaofuatwa lakini sisi Takukuru hatutakubali nchi iwakilishwe na wala rushwa,” alisema...... kwa taarifa zaidi soma www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment