Friday, April 27, 2012

MOHAMED MTONGA: HAKUTATOKEA UBADHIRIFU TENA WIZARA YA FEDHA


NA MWANDISHI WETU
WIZARA ya Fedha nchini imesema baada ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), kubaini matumizi mabovu ya mishahara hewa na mikataba mibovu, wizara hiyo haitarajii kujitokeza tena kwa ubadhirifu huo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Mohamed Mtonga wakati akifufunga semina ya siku nne ya maodita wa ndani jijini Dar es Salaam leo.
Alisema lengo la semina kwa washiriki hao ili kuwa ni kuwajengea uwezo ambao utawasaidia katika kazi zao haswa kudundua maeneo hatarishi ya upotevu wa fedha.
Mtonga alibainisha kuwa mafunzo hayo yawasaidia kubaini matumizi yasiyo ya kawaida kwa haraka kwa kuwa wizara imeanzisha mfumo mpya kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa njia ya kompyuta.
Alisema teknolojia hiyo ya kisasa ambayo inauwezo wa kugundua makosa hayo haraka katika maeneo mbalimbali, hivi sasa inatumiaka katika nchi ya Kenya ambapo imefanikiwa kwa kiwango cha juu.
Mtonga alisema kutokana na mafanikio ya nchi hiyo, Tanzania imeamua kuwapeleka maodita wake wanne (4), kwenda kujifunza teknolojia hiyo ambapo itaanza kutumika hivi karibuni hapa nchini.
Aidha, alisema Wizara ya Fedha imetoa muongozo unaowataka kila Katibu Mkuu wa Wizara kufanya uchunguzi katika kubaini maeneo hatarishi katika ofisi zao kitendo kitakacho wasaidia kugundua haraka ubadhirifu wa mishahara hewa na mikataba bandia kwa kutumia teknolojia hiyo.
Cheo hicho cha Mkaguzi Mkuu wa Ndani kimeanzishwa kisheria hivi karibuni kwa ajili ya kuboresha na kuongeza nguvu katika kazi za ukaguzi wa fedha ambapo hapo awali hakikuwepo.

No comments:

Post a Comment