![]() Daniel Mjema, Dodoma, Geofrey Nyang'oro Dar MKAKATI wa kukusanya majina 70 ya wabunge kama sehemu ya kukamilisha utaratibu wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, umepamba moto na hadi kufikia jana jioni, wabunge 75 walikuwa wameunga mkono hatua hiyo, watano kati yao, wakitokea chama tawala CCM. Endapo mchakato huo utakamilika, Pinda atakuwa ameingia katika historia ya kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na Bunge, tangu Tanzania ipate uhuru wake Desemba 9, 1961 Hata hivyo wakati mchakato huo ukiendelea, Spika wa Bunge, Anne Makinda jana jioni aliibuka bungeni na kueleza kuwa mchakato huo ni batili. Akinukuu vifungu vya Kanuni za Bunge na Katiba, Spika Makinda alisema mkakati huo ni batili kwa kuwa kanuni zinaeleza bayana kuwa ulipaswa kufanyika siku 14 kabla ya kuwasilisha hoja hiyo kwa Spika. "Bunge letu linaisha Jumatatu ambayo ni siku nne tu tangu leo (jana) na kwa mujibu wa kanuni, taarifa ya maandishi iliyotiwa saini na kuungwa na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote, itatolewa kwa Spika siku angalau 14 kabla ya siku inapokusudiwa kuwasilishwa bungeni." Spika Makinda alisema pamoja na hayo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe aliyeongoza mchakato wa kukusanya saini hizo za wabunge, alikuwa sahihi kuendesha mpango huo kwa mujibu wa Kanuni ya 133 ya Bunge na Ibara ya 53 (3)ya Katiba. Akizungumza na gazeti hili, Zitto alipingana na maelezo hayo ya Spika akidai kuwa aliyatoa kwa lengo la kutetea Serikali ya chama chake kwa kupindisha sheria. "Spika hajasema kitu, wamejipanga tu hawa (CCM). Sisi hatujampelekea hoja yetu. Tunampelekea Jumatatu kisha ataamua. Ili mradi iwe siku 14 kabla ya siku ya kutoa hoja. Wanaweweseka tu," alidai Zitto. Alifafanua; "Kanuni inasema siku 14 kabla, sisi tunakusanya saini ili tutimize sharti la kanuni. Spika anajaribu kulindaa Serikali ya chama chake kwa kupindisha kanuni." Kanuni zinasemaje Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, kipengele cha 133 (4) na (5) kuhusu hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kinaeleza: "Hoja inayotolewa chini ya kanuni hii na iliyotimiza masharti ya katiba itawasilishwa bungeni mapema iwezekanavyo na itaamuliwa kwa kura za siri." Kifungu cha tano kinasema kuwa hoja hiyo itapitishwa tu pale itakapoungwa na wabunge wengi. kanuni hizo za Bunge zinafafanua katika kifungu cha sita kuwa kama wabunge watapitisha hoja, itambidi Spika kuwasilisha azimio hilo kwa rais mapema iwezekanavyo. Kifungu hicho kinafafanua kwamba kwa namna yoyote ile ndani ya siku mbili, Waziri Mkuu atakuwa amejiuzulu na Rais kumteua mbunge mwingine kushika nafasi hiyo. Kwa mujibu wa Katiba, mpango wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu inafafanuliwa na Ibara ya 53. Kwenye ibara hiyo kifungu kidogo cha tatu kinatoa masharti ambayo wabunge wanapaswa kuyakamilisha ili kutekeleza azma yao ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.zaid soma www.mwananchi.com |
Saturday, April 21, 2012
Mkakati wa kumng'oa Pinda waiva
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment