Tuesday, March 27, 2012

Zitto Aivuruga CHADEMA Kugombea Urais 2015


Na mwandishi wetu
SIKU moja baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) Zitto Kabwe kutangaza nia ya kugombea urais mwaka 2015, kauli hiyo imewachanganya watendaji wakuu wa chama hicho, Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa.

Wakati Dk Slaa akikosoa hatua hiyo na kusema sio wakati mwafaka sasa kuzungumzia urais, Mbowe amesema hana tatizo na Zitto kutangaza nia hiyo sasa kwa kuwa ni haki yake, lakini akahoji haraka ya kutangaza dhamira hiyo.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti viongozi hao wamemshauri Zitto kufuata taratibu za chama kama anataka kufikia malengo yake hayo ya kutaka kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa taifa.

Kauli ya Dk Slaa
Akizungumzia uamuzi huo wa Zitto kutangaza dhamira hiyo, Dk Slaa alisema suala la urais sio muhimu kwa sasa kwani chama kinaangalia ushindi kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki.

"Naomba niseme hivi, sasa urais sio ‘issue’ (suala). Chama kinaangalia uchaguzi wa Arumeru Mashariki, muda wa kuzungumzia urais ukifika, tutasema," alisema Dk slaa na kuongeza:

“…Naomba mtambue kwamba tunakabiliwa na suala kubwa la uchaguzi huku Arumeru kwa hiyo sasa siwezi kuzungumzia suala la urais, hili sio wakati wake sasa.”

Hata hivyo alimshauri Zitto kufuata taratibu kama ana nia ya kugombea urais na kufafanua kwamba, chama kina utaratibu wake na ndicho chenye uamuzi wa mwisho.

“Chadema ina utaratibu wake kwa kila jambo, kama Zitto ametangaza kugombea urais 2015 huo ni uamuzi wake binafsi. Lakini mimi kama kiongozi wa chama sioni kama urais ni jambo la kujadili wakati huu.

“Ikifika wakati wakujadili masuala ya urais, tutafanya hivyo kwa undani lakini, sio kwa sasa kwani wakati wake haujafika.”

Mbowe
Kwa upande wake Mwenyekiti Mbowe, alisema kila mtu ana busara na haki zake katika kuamua jambo na hii, ni busara yake Zitto.

Lakini, Mbowe alionyesha kushangazwa na Zitto kutangaza nia hiyo sasa wakati ambao chama kinawaza na kufikiria uchaguzi wa Arumeru Mashariki.

Mbowe alisema haoni tatizo Zitto kutangaza sasa nia ya kuutaka urais kwa kuwa ni uamuzi na haki yake kwasababu kila mwanachama wa Chadema ana haki ya kuamua jambo analolitaka ili mradi afuate taratibu.

“Sioni kama Zitto ana tatizo lolote la kutangaza sasa kwamba mwaka 2015 anataka kugombea urais kwani ni haki ya kila mtu kugombea nafasi hiyo,” alisema Mbowe

Hata hivyo, alifafanua kwamba pamoja na Zitto kutangaza nia, wakati wa kuwania nafasi hiyo ndani ya chama ukifika wanachama wa Chadema ndio watakaotoa uamuzi wa nani anafaa.Soma zaidi http://www.mwananchi.co.tz/

No comments:

Post a Comment