Wednesday, March 28, 2012

Zaidi ya watu 280 Wilayani Kilolo mkoani Iringa wagundulika kuwa na kifua kikuu

 
Picha hii ikionyesha moja ya matukio ya upimaji wa afya huko Songea mkoani Ruvuma.
Zaidi ya wagonjwa 280 kwa mwaka 2011 Wilayani kilolo Mkoani Iringa wamegundulika kuwa na kifua kikuu ambapo kati yao wagonjwa 247 sawa na asilimia 86 walipima maambukizi ya virusi vya ukumwi, kati yao wagonjwa 126 sawa na asilimia 51 walikuwa na maambukizi yote yaani kifua kikuu pamoja na  ukimwi.
 Tathmini hiyo imetolewa na Mganga Mkuu Wilaya ya Kilolo Wilfred Rwechungura huku akizitaja sababu mbalimbali zinazopelekea maambukizi ya ugojwa wa kifua kikuu katika wilaya ya kilolo.
 Naye diwani wa kata ya Ilole Mheshimiwa John mkonda amesema kuwa katika kupunguza kasi ya maambukizi ya kifua kikuu, Wananchi wilayani Kilolo Mkoani Iringa wanatakiwa kuacha tabia ya Kuchangia chombo kimoja wakati wa kunywa pombe wakiwa kilabuni, kwani imeonekana kuwa moja ya sababu zinazopelekea maambukizi ya kifua kikuu (TB) wilayani himo.
 Nae Mkurugenzi wa Wilaya hiyo Bosco Ndungulu amewaambia wananchi kuwa ugonjwa huo unatibiwa bure hivyo wanapaswa wananchi wa kilolo kutoufumbia macho ugonjwa huo kwa kupata tiba sahihi mapema kwani ugonjwa huo ukiugundua mapema unatibika pasipo pingamizi lolote endapo tu Mgonjwa atafuata ushauri wa daktari na kumaliza dozi.
 Akitoa ushuhuda kwa wanakilolo mmoja wa watu ambao waliwahi kuugua ugonjwa huo Simon Mmehe, amesema kuwa ugonjwa huo unatibika hata yeye alipona na anaafya nzuri hivyo wananchi wanapaswa kutokuwa na hofu.
 Aidha maadhimisho ya kifua kikuu na ukoma duniani hufanyika machi 24 kila mwaka ambapo mwaka huu halmashauri ya wilaya ya kilolo imefanya ,maadhimisho hayo katika kijiji cha Lundamatwe, kata ya Ilole mkoani Iringa huku kauli mbiu ikiwa ni „nitatokomeza kifua kikuu kipindi chote cha uhai wangu“.

No comments:

Post a Comment